Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la COVID-19 limepindua ulimwengu wa ajira

Wafanyakazi wakiwanda  huko Cambodia
ILO/Marcel Crozet
Wafanyakazi wakiwanda huko Cambodia

Janga la COVID-19 limepindua ulimwengu wa ajira

Ukuaji wa Kiuchumi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19, limepindua ulimwengu wa ajira na kusisitiza kuwa, “hali ya sasa haipaswi kusalia kama ilivyo baada ya janga hili kupita.”

Katika ujumbe wake wa kisera aliotoa kwa video hii leo, Guterres amesema ajira milioni kadhaa zimepotea hususan kwenye uchumi usio rasmi na wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ndio wanaokumbwa na shida zaidi.

“Janga hili kwenye ulimwengu wa dunia limeongeza mafuta kwenye moto wa kutoridhika na shaka na shuku ambao tayari ulikuwa unawaka. Kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira na kupotea kwa vipato kutokana na COVID-19, kunaongeza mmomonyoko wa kijamii na kuondoa utulivu kwenye mataifa na maeneo, kijamii, kisiasa na kiuchumi,” amesema Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema wakati kampuni na wafanyakazi wanatumia mbinu bunifu kubadili mazingira, “wale walio hatarini zaidi wanazidi kuwa hatarini, na nchi maskini na jamii maskini zinazidi kusalia nyuma zaidi.”

Katika wito wake huo wa kisera, Katibu Mkuu Guterres anataka hatua zaidi na za haraka zichukuliwe ili kusaidia wafanyakazi, kampuni na ajira ambazo ziko hatarini zaidi ili kuepusha kufungwa kwa maeneo hayo, kupotea kwa ajira na vipato.

“Kunapaswa kuwepo kwa umakini zaidi kwenye afya na uchumi baada ya kulegezwa kwa masharti yatokanayo na COVID-19, maeneo ya kazi yaliyo salama, na haki za wanawake na jamii zilizo hatarini,” amesema Katibu Mkuu.

Ameongeza kuwa, “tunahitaji kuhamasisha sasa mipango ya kujikwamua ambayo inazingatia ubinadamu, endelevu na isiyoharibu mazingira na kutumia teknolojia za kisasa za kuunda ajira zenye utu kwa wote na kutumia ubunifu wa kampuni na wafanyakazi ambao unatumika zama hizi.”

Bwana Guterres amesema kabla ya COVID-19, dunia haikuwa ya kawaida kwenye masuala ya ongezeko la ukosefu wa usawa, ubaguzi wa kimfumo  kabisa wa kijinsia na ukosefu wa fursa kwa vijana, viwango vya mishahara visivyoongezeka na madhara ya mabadaliko ya tabianchi na kwamba janga la Corona limefichua zaidi zahma zitokanazo na changamoto hizo, utete na nyufa.

Amesisitiza kuwa, “ni wakati wa kuratibu juhudi za kimataifa, kikanda na kitaifa ili kuweka mazingira ya ajira zenye utu na zisizoharibu mazingira na kujikwamua ambako ni shirikishi na wenye mnepo. Mathalani kuondokana na kutoza kodi mishahara na badala yake kodi ielekezwe kwenye nishati ya hewa ya ukaa na hii inaweza kusaidia kwa muda mrefu.”

Amesisitiza kuwa kwa hatua safi katika ngazi zote, na kwa kuzingatia ajenda ya 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu, “tunaweza kuibuka kutoka katika janga hili tukiwa thabiti, na wenye ajira bora zaidi na mustakabali bora na wenye usawa na uchumi usioharibu mazingira.”