Ingawa mimi ni mkimbizi lakini Kakuma ni nyumbani:Nhial Deng

19 Juni 2020

Kutana na Nhial Deng mkimbizi kutoka Sudan Kusini anayeishi katika moja ya kambi kubwa ya wakimbizi ya Kakuka nchini Kenya. Leo anatueleza jinsi siku yake inavyokua na anavyojilinda na janga la COVID-19.

Nhial Deng safari yake ya ukimbizi ilianza baada ya wazazi wake kufungasha virago wakati huo Sudan na kukimbilia Ethiopia ambako alizaliwa. Na mashambulizi katika Kijiji chao yalimfanya akafunga safari na kukimbia, safari hii peke yake akiwa na umri mdogo sana na kuishia kwenye kambi ya Kakuma Kenya ambako aliwekwa familia moja iliyomlea.

“Leo nakukaribisha ushiriki siku nami Kakuma na ujue nini tunachokifanya kujilinda sisi na jamii inayotuhifadhi dhidi ya virusi vya corona”

Ingawa alipitia changamoto nyingi Nhial mwenye miaka 21 hivi sasa anasema elimu ndio inayompa matumaini. lakini Je siku yake inaanza vipi?

“Kila siku naamka saa kumi na moja na dakika 45 alfajiri , natumia dakika 15 kutafakari na kisha kuoga tayari kuianza siku, baada ya hapo nasoma kwa muda wa saa moja na nusu. Kuwa na utaratibu kwangu ni muhimu sana kwa sababu unanisaidia kuwa na stamena na mawazo maruzi.”
Kambi ya Kakuma ina karibu wakimbizi 200,000, wanajilinda vipi na janga hili la corona au COVID-19?

“Tuna vituo vya kunawa mikono kwenye lango kuu ili kila mtu anayekuja aweze kunawa mikono na kila anayeondoka aoshe mikono pia. Na lazima nivae barakoa yangu vizuri.”

Anasema hata maduka yyote yana sehemu za kunawa mikono kuhakikisha wateja wananadumish usafi wanapoingia na kutoka.

Nihial hupata fursa pia ya kwenda mjini kwenye mtandaoni wa intaneti ili kusoma barua pepe zake, kuchapisha vitu vya shule na kuwasiliana na marafiki zake. Saa zinayoyoma muda wa kurejea nyumbani umewadia kupumzika na kisha kufanya mazoezi ya kukimbia. Na ana ujumbe kwa dunia kuhusu corona
“Ujumbe wangu kwa dunia ni kwamba hebu tupambane na janga hili pamoja na tusimwache yeyote nyuma, kwa sababu hakuna hata mmoja wetu atakayekuwa salama hadi wote tutakapokuwa salama.”

Hivi sasa Nihial ni mchagizaji wa masuala ya elimu, mfanya kampeni ya masuala ya vijana na anajitolea katika program mbalimbali kambini hapo.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud