Tunao wajibu wa kutekeleza ahadi ya kutokomeza migogoro-Guterres

19 Juni 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake wa siku ya wakimbizi duniani ameeleza ahadi ya Umoja wa Mataifa kukomesha migogoro na mateso yanayosababisha mamilioni ya watu kuwa wakimbizi.

Bwana Guterres amesema kuwa Umoja wa Mataifa unaahidi kufanya kila lililo katika uwezo wake kukomesha migogoro na mateso ambayo imesababisha takribani watu milioni 80 wanawake, watoto na wanaume kote duniani kuyakimbia makazi yao na kujikuta ukimbizini.

Akifafanua ukubwa wa tatizo hili, Guterres amesema cha kutisha zaidi ni kuwa watu milioni 10 kati ya hawa, waliyakimbia makazi yao katika mwaka mmoja pekee uliopita.

Aidha ameutumia ujumbe wake huu kuzishukuru nchi na jamii ambazo zinawapokea wakimbizi licha ya kuwa nazo zina mahitaji.

UN Photo/John Isaac
Wakimbizi wa Rwanda ambao waliikimbia nchi wakati wa mauaji ya kimbari, katika picha walipokuwa wakirejea nyumbani.

“Leo, pia tunatambua ukarimu na ubinadamu wa jamii wenyeji na nchi ambazo mara nyingi zinakabiliwa na wasiwasi wa kiuchumi na kiusalama. Tunastahili kuzipatia nchi hizi shukrani, usaidizi wetu na uwekezaji.”

Akizungumzia namna ugonjwa wa COVID-19 unavyoongeza tishio kwa wakimbizi Bwana Guterres amekumbushia taarifa ya sera aliyoieleza hivi karibuni kuhusu COVID-19 kwamba alitoa wito kwa serikali kote duniani kuwahusisha katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo watu walioko katika hatua za kuhama au ukimbizini.

Vile vile Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameutambua pia mchango wa wakimbizi na waliofurushwa makwao kwamba baadhi yao pamoja na kuwa wakimbizi lakini wamekuwa wakifanya kazi kama nesi, daktari, wanasayansi, walimu na pia kurejesha fadhila kwa jamii zinazowapokea.

“Katika siku hii ya wakimbizi duniani, tunawashukuru wakimbizi kwa urasilimali wao na uamuzi wa kujenga upya maisha yao na kuboresha Maisha ya wale wanaowazunguka. Leo na kila siku tunasimama kwa umoja na mshikamano na wakimbizi na kutambua jukumu letu la msingi la kuwalinda wanaokimbia vita na mateso.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud