Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 1 ya watu wote duniani wamelazimika kukimbia makwao: UNHCR

Mama akimtunza mtoto wake ndani ya mahali mazoezi ambapo pamegeuzwa kuwa makazi ya wakimbizi huko Pintolandia, Brazil.
©UNHCR/Vincent Tremeau
Mama akimtunza mtoto wake ndani ya mahali mazoezi ambapo pamegeuzwa kuwa makazi ya wakimbizi huko Pintolandia, Brazil.

Asilimia 1 ya watu wote duniani wamelazimika kukimbia makwao: UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Ripoti mpya ya mwenendo wa kimataifa wa wakimbizi na watu waliotawanywa duniani ambayo imetolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR inasema asilimia moja ya watu wote duniani wamelazimika kufungasha virago na kukimbia makwao kwa sababu moja au nyingine.

Kupitia ripoti hiyo UNHCR imetoa wito kwa nchi zote duniani kujitahidi zaidi kuwapa makazi mamilioni ya wakimbizi na watu wengine waliotawanywa na vita, mauaji, au vitendo vingine vya kuvuruga amani na utulivu wa umma.

Kwa mujibu wa UNHCR ripoti hii iliyotolewa leo inaonyesha kwamba “kwa mara ya kwanza kutawanywa kwa lazima kuwewaathiri asilimia moja ya watu wote duniani sawa na mtu 1 katika kila watu 97 huku watu wanaoweza kurejea makwao idadi inazidi kuwa ndogo.”

Ripoti hiyo ya kila mwaka ya UNHCR ambayo imetolewa siku mbili kabla ya siku ya wakimbizi duniani itakayokuwa Juni 20 inasema mwaka 2019 watu waliolazimika kutawanywa kote duniani ilikuwa milioni 79.5 ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa.

Ripoti pia inaonyesha kupotea kwa matarajio ya wakimbizi linapokuja suala la matumaini ya kumalizika kwa madhila yao.  

Katika miaka ya 1990 kwa wastani wakimbizi milioni 1.5 waliweza kurejea nyumbani kila mwaka lakini katika muongo uliopita idadi hiyo imepungua na kufikia takriban watu 385,000.

Mama na mwanawe huko Cox's Bazar kambi ya wakimbizi ya Balukhali
UN Women/Allison Joyce
Mama na mwanawe huko Cox's Bazar kambi ya wakimbizi ya Balukhali

Akifafanua kuhusu ripoti hiyo Kamisha mkuu wa wakimbizi Filippo Grandi amesema “Tunashuhudia mabadiliko ya hali halisi kwa watu wanaotawanywa kwamba leo hii hilo sio tu ni tatizo kubwa lililosambaa bali pia sio tatizo la muda mfupi tena .Watu hawawezi kutarajia kuishi katika hali ya sintofahamu kwa mika mingi bila fursa ya kurejea nyumbani wala matumaini ya kujenga mustakbali wao mahali waliko. Kimsingi tunahitaji mtazamo mpya na wa ukarimu kwa watu ambao wanakimbia,ambao utakuwa na lengo la kutatua migogoro ya muda mrefu ambayo ndiyo chanzo cha madhila makubwa kwa watu hawa.”

Ripoti inasema ongezeko la watu waliotawanywa kutoka milioni 70.8 mwishoni mwa mwaka 2018 ni matokeo ya sababu kuu mbili .

Mosi ni hali mpya ya kuogopesha ya idadi kubwa ya watu waliotawanywa mwaka 2019 hususani nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC, Sahel, Yemen na Syria ambayo sasa iko katika mwaka wa kumi wa vita ambayo pekee ina wakimbizi, waomba hifadhi na wakimbizi wa ndani milioni 13.2 idadi ambayo ni moja ya sita ya idadi yote ya dunia.

Pili ni hali ya uwakilishi wa Wavenezuela walio nje ya nchi ambao hawajaorodheshwa rasmi  kama wakimbizi au waomba hifadhi lakini wanahitaji mipango ya kuwalinda.

Ripoti imeweka bayana kwamba katika idadi yote hiyo watoto wanakadiriwa kuwa kati ya milioni 30 hadi 34 na maelfu kati yao wako peke yao bila wazazi au walezi.