Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usivae barakoa wakati unafanya mazoezi-WHO

Vijana wakiwa wamevaa barakoa wakati wa kuendesha baiskeli kwenye bustani moja huko Büyükçekmece, Uturuki.
UNDP/Levent Kulu
Vijana wakiwa wamevaa barakoa wakati wa kuendesha baiskeli kwenye bustani moja huko Büyükçekmece, Uturuki.

Usivae barakoa wakati unafanya mazoezi-WHO

Afya

Wakati ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 ukiendelea kuenea katika maeneo mbalimbali duniani huku kwingine ukiwa unadhibitiwa, shirika la afya la Umoja wa Mataifa, linaendelea kutoa madokezi kadhaa ili kuhakikisha kuwa mbinu za kujikinga dhidi ya ugonjwa huo hazigeuki na kuwa mwiba kwa mhusika.
 

Miongoni mwa mbinu zinazotumiwa sana hivi sasa ni uvaaji wa barakoa ambapo baadhi ya watu wameonekana wakivalia barakoa hizo hata wakati wanakimbia au wakifanya mazoezi.

WHO kupitia kipeperushi chake inasema kuwa, “watu hawapaswi kuvaa barakoa wakati wanafanya mazoezi kwa sababu barakoa inaweza kumzuia kuvuta pumzi vizuri.”

WHO inasema kuwa jasho kutoka kwa mvaaji wa barakoa linaweza kulowesha barakoa hiyo na “kufanya iwe vigumu kuvuta pumzi na pia kuweka mazingira mazuri kwa vijiumberadhi.”

Je anayefanya mazoezi afanyeje?

Shirika hilo linasema njia bora zaidi wakati unafanya mazoezi ni kuhakikisha kuwa “unazingatia umbali unaotakiwa angalau mita moja kutoka kwa mtu mwingine. Zingatia kutochangamana.”

Tafadhali bofya hapa kupata taarifa zaidi kuhusu aina za mazoezi unazoweza kufanya wakati huu wa COVID-19.