Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubaguzi wa rangi unakiuka katiba ya UN na msingi wa maadili yetu:UN

George Floyd, Mmarekani mweusi aliyeuaw baada ya kukamatwa na polisi nchini Marekani
UN News/Daniel Dickinson
George Floyd, Mmarekani mweusi aliyeuaw baada ya kukamatwa na polisi nchini Marekani

Ubaguzi wa rangi unakiuka katiba ya UN na msingi wa maadili yetu:UN

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa umesema ubaguzi wa rangi na ubaguzi wa aina yoyote ile unakiuka katiba ua Umoja wa Mataifa na msingi wa maadaili yake na hivyo hauna nafasi katika karne hii.

Akizungumza kwa njia ya video kwenye mjadala wa dharura na wa lazima wa Baraza la Haki za Binadamu hii leo uliofanyika mjini Geneva naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi. Amina J. Mohammed amemnukuu Katibu Mkuu wa umoja wa Mataifa akisema “Msimamo wa Umoja wa Mataifa kuhusu ubaguzi wa rangui uko bayana, jinamizi hili linakiuka katiba ya Umoja wa Mataifa na kumomonyoa maadili ya msingi wake.”
Pia amesema Katibu mkuu ametoa wito wa kukomesha mifumo ya ubaguzi wa rangi na kukabiliana na taratibu za kibaguzi zilizomea mizizi katika taasisi mbalimbali.

Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J Mohammed (Maktaba)
UN Photo/Manuel Elías
Naibu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J Mohammed (Maktaba)


Na kwa Umoja wa Mataifa amesema Katibu Mkuu amezindua mchakato wa mwaka mmoja wa kushughulikia shuku na shaka za wafanyakazi. Pia ametaka kuwepo na uwekezaji mkubwa katika mahusiano ya kijamii akisisitiza kuwa “Mchanganyiko katika jamii ni utajiri na si tishio.”

Naunga mkono yaliyosemwa na wenzangu

Bi. Mohammed pia ameweka wazi kwamba anaunga mkono yaliyosemwa na viongozi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ambao ni Waafrika au wenye asili ya Afrika katika taarifa yao iliyotolewa siku tatu zilizopita, ambapo walisisitiza kwamba “Hakuna kauli zitakazotosheleza kusema kuhusu madhila na machungu ambayo yamesababishwa na kutokuwepo haki na ubaguzi wa rangi kwa karne, hususan dhidi ya watu wenye asili ya Afrika. Kulaani tu kauli na vitendo vya ubaguzi wa rangi hakutoshi, ni lazima twende mbali zaidi na kufanya juhudi zaidi.”
Amina Mohammed amesema leo hii watu wanapaza sauti zao na kusema wazi kwamba “imetosha” na Umoja wa Mataifa una wajibu wa kuchukua hatua kwa madhila ambayo yamekuwa yakiwakumba watu kwa miaka mingi na hili liko katika kitovu cha taswira ya umoja wa Mataifa, kwani haki sawa kwa wote zimejumuishwa katika katiba iliyounda umoja wa Mataifa.

Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu.
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu.

 

Kamishina Mkuu wa Haki za Binadamu

Kwa upande wake Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ametoa wito wa kuwepo kwa hatua za uwajibikaji zaidikwa vikosi vya usalama. Mjadala wa dharura ulipendekezwa nan chi za afrika baada ya mauaji ya George Floyd mnamo Mei 25 alipokuwa amekamatwa na polisi mjini Minneapolis nchini Marekani.

Mkutano huu unafanyika katika kikao cha 40 cha Baraza la Haki za binadamu kuhusu masuala yanayochochewa na ubaguzi wa rangi, ukatili wa polisi dhidi ya watu wenye asili ya afrika na ukatili dhidi ya watu wanaoandamana kwa amani.

Katika mkutano huo Bi. Bachelet amesisitiza “Kuchukuliwa kwa hatua Madhubuti duniani kote za kufanyia mabadiliko au kuanzisha vyombo na taasisi za kisheria , na kushughulikia kusambaa kwa ubaguzi wa rangu.”

Mzunguko

Bi. Bachelet amesisitiza kwamba “Maisha ya watu weusi ni muhimu, Maisha ya watu wa asili ni muhimu na maisha ya watu wa rangi mbalimbali ni muhimu.
Ameongeza kuwa “Ubaguzi wa rangi umeharibu taasisi za serikali, kupinga usawa na kusababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na hivyo ni wa kati wa kukomesha mzunguko huu na ukwepaji sheria.

Philonise Floyd,kaka wa hayati George Floyd akizungumza kwa njia ya video kwenye mjadala wa Baraza la Haki za Binadamu
UN Geneva
Philonise Floyd,kaka wa hayati George Floyd akizungumza kwa njia ya video kwenye mjadala wa Baraza la Haki za Binadamu

 

Kaka wa Floyd

Miongoni mwa waliohudhuria na kuzungumza kwa njia ya mtandao kwenye mjadala huo ni makamu wa Rais wa tume ya Muungano wa Afrika Kwesi Quartey na kaka wa hayati George Floyd.

Akihutubia mjadala huo Philonise Floyd ameliomba baraza la haki za binadamu kuunda tume huru kuchunguza mauaji ya Wamarekani weusi yanayotokea mikononi mwa polisi nchini Marekani lakini pia machafuko na ukatili dhidi ya watu wanaoandamana kwa amani.

Kuhusu maandamano Philonise ametaja kwamba “wakati watu wakijitoa kupaza sauti zao na kuandamana kwa ajili ya kaka yake walirushiwa mabomu ya kutoa michozi au kukanyagwa na magari ya polisi. Kuna watu ambao wameumia ikiwemo kuathirika ubongo baada ya kupigwa na risasi za mpira.
Pia kwenye mjadala huo kulikuwepo uwakilishi wan chi mbalimbali, mashirika yasiyo ya kiserikali NGO.s na mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu ubaguzi wa rangi Tendayi Achiume ambaye amezungumza pia. Baraza hili linatarajiwa kutoa na azimio liytakalopitishwa hapo kesho Alhamisi.