Skip to main content

Afya ya binadamu inategemea afya ya sayari tunayoishi:Guterres

Msichana akipika katika moja ya vijiji nchini Ethiopia ambalo ardhi imeathirika vibaya na ukame unaoendelea
© UNICEF/Tanya Bindra
Msichana akipika katika moja ya vijiji nchini Ethiopia ambalo ardhi imeathirika vibaya na ukame unaoendelea

Afya ya binadamu inategemea afya ya sayari tunayoishi:Guterres

Tabianchi na mazingira

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kukabiliana na ongezeko la jangwa na ukame duniani Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameisihi dunia kulinda ardhi ya sayari tunayoishi kwani afya ya binadamu inategemea afya ya sayari hiyo.

Kupitia ujumbe wake wa siku hii Guterres amesema leo hii dunia inateketea, mmomonyoko wa ardhi unawaathiri watu bilioni 3.2 na asilimia 70 ya ardhi ya duniani imebadilishwa na shughuli za kibinadamu.

Katibu Mkuu amesema hali hii inaweza kubadilishwa na kuleta suluhisho ya changamoto nyingi zinazoikabili dunia kuanzia uhamiaji wa kulazimishwa, njaa hadi mabadiliko ya tabia nchi.

Sehemu kame katika eneo lenye hali ya nusu jangwa huko Tera, Niger baranai Afrika
©FAO/Giulio Napolitano
Sehemu kame katika eneo lenye hali ya nusu jangwa huko Tera, Niger baranai Afrika

Katika eneo la Afrika la Sahel, amesema ukanda mkubwa wa Kijani-Kibichi unabadilisha maisha na njia za watu kuishi kutoka Senegal hadi Djibouti na kuongeza kuwa "Kwa kurejesha katika ubora ekari milioni 100 za ardhi iliyoharibiwa, uhakika wa chakula unadumishwa, kaya zinahifadhiwa na ajira zimetengenezwa. Juhudi kama hizo zinarudisha bayoanuai, hupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi na kufanya jamii kuwa na mnepo zaidi. Kwa ujumla, faida zinazidi gharama mara kumi."

Pia katika kuadhimisha siku hii ya kukabili Jangwa na Ukame, ametoa wito wa kuwa na mkataba mpya kwa ajili ya masuala ya asili

"Kupitia hatua ya kimataifa na mshikamano, tunaweza kuongeza urejeshwaji wa ardhi na suluhisho la asili kwa hatua za kukabili mabadiliko ya tabianchi na faida kwa vizazi vijavyo. Kwa kufanya hivyo, tunaweza kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu na kuhakikisha hakuna mtu atakayeachwa nyuma.”.

Siku ya kimataifa ya kukabiliana na ongezeko la jangwa na ukame huadhimishwa kila mwaka Juni 17.