Bei ya dozi ya chanjo ya ‘Numonia’ yapungua kwa asilimia 43 

Muuguzi katika kituo cha afya cha Elmina nchini Ghana akiweka katika bomba la sindano chanjo dhidi ya homa ya vichomi au numonia.
© UNICEF/Nyani Quarmyne
Muuguzi katika kituo cha afya cha Elmina nchini Ghana akiweka katika bomba la sindano chanjo dhidi ya homa ya vichomi au numonia.

Bei ya dozi ya chanjo ya ‘Numonia’ yapungua kwa asilimia 43 

Afya

Hatimaye bei ya chanjo ya ugonjwa wa homa ya vichomi au Numonia, PVC,  imeshuka kwa asilimia 43 na kufikia dola 2 za kimarekani kwa dozi moja na hivyo kuwa ni nafuu kubwa kwa nchi za kipato cha chini duniani kote.

Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF iliyotolewa katika miji ya New York, Marekani na Geneva, Uswisi imesema kuwa punguzo hilo linafuatia makubaliano mapya kati ya UNICEF na taasisi ya Serum nchini India, SII.

Bei mpya ya dola 2 imepungua kwa asilimia 43 kutoka makubaliano ya awali ya soko, AMC, kwa bei ya fuko la chanjo duniani, GAVI iliyokuwa dola 3.50 za kimarekani.

Chanjo hiyo ni mwokozi mkubwa kwa watoto katika nchi maskini ambako ugonjwa wa homa ya vichomi ni moja ya sababu kubwa ya vifo.

UNICEF inasema kuwa, “makubaliano haya ya usambazaji na bei ni ya nane kufanyika na ya kwanza kujumuisha kampuni ya kutengeneza dawa kutoka nchi inayoendelea. Kwa mujibu wa mkataba, kampuni ya dawa ya India itapatia mataifa yanayopata msaada kutoka Gavi, dozi milioni 10 za chanjo dhidi ya homa ya vichomi kila mwaka kwa kipindi cha miaka 10 ijayo.”

Makubaliano ya awali ya bei sokoni, AMC yaliyopo hivi sasa kwa bei hiyo ya dola 3.50 yanamalizika mwishoni mwa mwaka huu na yalizinduliwa mwaka 2009 kwa msaada wa wahisani kutoka Uingereza, Canada, Urusi, Norway na taasisi ya Bill na Melinda Gates kwa lengo la kuondoa uhaba wa chanjo kwenye nchi maskini.

Bila makubaliano kama hayo, chanjo kama ya Numonia inaweza kufikia nchi maskini ambazo zina mzigo zaidi wa gonjwa hilo kati ya miaka 10 hadi 15 tangu kutengenezwa kwake.

Mtoto akipata chanjo dhidi ya homa ya vichomi kwenye kituo cha afya cha Makuru nchini Kenya.
© UNICEF/Shehzad Noorani
Mtoto akipata chanjo dhidi ya homa ya vichomi kwenye kituo cha afya cha Makuru nchini Kenya.

Kwa hiyo AMC ambacho huchagiza tafiti na maendeleo ya chanjo ni mkombozi kwa sababu huwezesha kutengenezwa kwa dawa za kukidhi mahitaji na uwezo wa kifedha wa nchi za kipato cha chini.

Chini ya AMC, chanjo hiyo ya vichomi au numonia imefikia zaidi ya nchi 60 za kipato cha chini ambako kiwango cha utoaji wa chanjo hiyo ni asilimia 48, kiwango ambacho ni cha juu kuliko kile cha wastani cha asilimia 47 duniani kote.

 Akizungumzia hatua hii mpya, Mkurugenzi wa UNICEF anayehusika na usambazaji na manunuzi Etleva Kadili amesema kuwa, “Numonia ni muuaji mkubwa wa watoto, ikisababisha kifo cha mtoto mmoja kila katika sekunde 39. Kwa kuweza kupeleka chanjo hiyo au PVC kwa bei nafuu, tunaweza kuokoa maisha ya mamilioni ya watoto. Mfumo wetu bunifu umepatia motisha wazalishaji kutuletea chanjo hii kwa uwezo wa soko.”

Amesema kuwa hiyo ina maana kwamba nchi nyingi zaidi, zikiwemo zile za kipato cha kati ambazo bado hazijajumuisha chanjo hiyo katika ratiba yao chanjo kutokana na bei, kuwa na fursa ya kuijumuisha sasa kwa ajili ya watoto wote.

Wakati wa mkutano wa chanjo wa kimataifa wiki iliyopita, Gavi ilizindua ahadi ya kusaka chanjo dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19, ikiwa ni kichocheo kwa wazalishaji kuzalisha kiwango cha kutosha cha chanjo hiyo itakapopatikana ili hatimaye iweze kufikia pia nchi zinazoendelea.