8 Juni 2020

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, limetoa mwongozo mpya wa matumizi ya barakoa katika harakati za kuepusha maambukizi zaidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.
 

Mwongozo huo (bofya haya kuupata) unaeleza bayana nani avae barakoa, wakati gani barakoa ivaliwe, mahali  gani ivaliwe na barakoa hiyo iwe imetengenezwa na kitu gani.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus akizungumzia mwongozo huo anasema kuwa, “katika maeneo ambamo kuna maambukizi miongoni mwa wanajamii, tunashauri kuwa watu wenye umri wa miaka 60 na kuendelea, au wale ambao wana magonjwa mengineyo, lazima wavae barakoa za kitabibu kwenye mazingira ambamo si rahisi kuepusha kutochangamana. Kwa kuzingatia ushahidi ambao unazidi kujitokeza, WHO inashauri serikali zihamasishe wananchi wake kuvaa barakoa pale ambako  kiwango cha maambukizi ni kikubwa na kutochangamana hakuwezi kufanyika.”

UNICEF/Bullen Chol
Muuza nyama akiwa amevalia barakoa yake katika duka lake la nyama huko sokoni KonyoKonyo mjini Juba ,nchini Sudan Kusini.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO amesema kuwa mwongozo huo mpya unataja pia aina ya kitambaa kinachopaswa kutumika kutengenezea barakoa lakini “katu barakoa si mbadala wa kuepuka kuchangamana, usafi wa mikono na mikakati mingine ya umma ya kiafya na kwamba zinafaa tu kwa ajili ya mkakati wa kina wa kuzuia kuenea kwa COVID-19

© UNICEF/Bullen Chol
Wananchi wa Sudan Kusini katika soko la Konyo Konyo mjini Juba wakijisomea taarifa kuhusu COVID-19 baada ya kupatiwa barakoa za kitambaa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi anayehusika na masuala ya dharura, WHO, Mike Ryan amesema kuwa, “ijapokuwa barakoa zinatumika kwa kiasi kikubwa katika nchi ambazo zimefanikiwa kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona, nchi hizo pia ziko mstari wa mbele katika kubaini wagonjwa wapya, kuchunguza maeneo hatarishi, kupima wananchi wake virusi vya Corona, kutenga wagonjwa na kuwaweka karantini waambata wa wagonjwa.”

Akisisitiza matumizi ya barakoa, mkuu wa masuala ya kiufundi WHO, Maria Van Kerkhove, amesema kuwa, “pale ambako kutochangamana hakuwezekaniki na hakuwezi kuzingatiwa, basi barakoa iwe isiyo ya kitabibu, ya kitambaa inapaswa kutumika na mwongozo wetu unaelezea kabisa aina ya kitambaa na jinsi ya kuishona.”
 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud