Pamoja na matumaini kuna hofu bado kwa watoto walio kwenye migogoro ya silaha:UN

15 Juni 2020

Umoja wa Mataifa umesema baina ya hofu na mashaka na matumaini kwa mamilioni ya Watoto walio katika nchi zenye migogoro ya silaha ni muhimu sana kutekeleza usitishwaji wa mapigano na michakato ya amani.

Akiwasilisha ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya 2019 hii leo kwenye Baraza la Usalama  kuhusu Watoto na mizozo ya silaha , mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kwa ajili ya watoto kwenye mizozo ya silaha Virginia Gamba amesema “Janga la wavula na wasicha kutumiwa na kufanyiwa ukatili kwenye mizozo ya silaha limeendelea kwa mwaka mzima wa 2019, huku Umoja wa Mataifa ukithibitisha na kuorodhesha zaii ya vitendo 25,000 vya ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto katika ripoti hiyo.”

Ameongeza kuwa kwa ujumla idadi ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za Watoto bado iko juu kama ilivyokuwa mwaka 2018 ambayo ni sawa na aina 70 za ukiukwaji kwa siku.

Watoto wakiwa kwenye kituo chao cha kucheza ambacho ni salama. Kituo kimeanzishwa na UNICEF.
© UNICEF/Sibylle Desjardins
Watoto wakiwa kwenye kituo chao cha kucheza ambacho ni salama. Kituo kimeanzishwa na UNICEF.

Watoto wameporwa utoto wao

Bi. Gamba ameliambia Baraza la Usalama kwamba “Utoto wa wavulana na wasicha hawa umeporwa na badala yake kupewa machungu, ukatili na hofu wakati dunia ikikodoa na kutazama kinachoendelea. Pandekinzani katika mizozo zinapuuza kuwalinda Watoto dhidi ya ukatili na zinawanyima msaada wa muhimu wanaouhitaji. Kwa kukiuka kanuni za vita pande hizo zinahatarisha maisha ya watoto wao.”

Cha kustua zaidi katika ripoti hiyo ni ongezeko kubwa la kukataliwa kwa fursa za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Watoto ambako kumeongezeka zaidi ya asilimia 400 ambapo matukio 4,400 ya aina hiyo yamethibitishwa.

Ripoti imeelezea pia ukatili dhidi ya wahudumu wa misaada ya kibinadamu na kuathiri kazi zao, uporaji wa vifaa na misaada na kuzuia wahudumu hao kutoka sehemu moja kwenda nyingine, miongoni mwa usumbufu na athari zingine dhidi ya utoaji wa misaada ya muhimu kwa watoto.

Maeneo yanayotia wasiwasi mkubwa

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Katibu Mkuu maeneo yanayotia wasiwasi mkubwa ni Pamoja na Yemen, Mali, Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Israel, Palestina na Syria.

Imeongeza kuwa kupuuza na kutoheshimu maeneo muhimu ya raia kama shule na hospitali kumesalia kuwa ni suala linalotia hofu kubwa huku yakiorodheshwa matukio 927 ya mashambulizi dhidi ya shule na hospitali hasa katika nchi za Afghanistan, Israel na Palestina na Syria.

Kwa ujumla Bi. Gamba amesema “Kwa ujumla mamilioni ya Watoto walikosa elimu na huduma za afya kutokana na mashambulizi, matumizi mabaya au kufungwa kwa shule sababu ya matumizi ya kijeshi. Wavulana na wasichana wanaendelea kukabiliwa na ukatili wa kingono ambapo visa 735 vimethibitishwa  hata hivyo inaonekana hali halisi ya ukiukwaji huo ni kubwa kuliko inavyoripotiwa. Idadi kubwa imeripotiwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Somalia na CAR”.

Amesema sababu kama ukwepaji wa sharia kwa watekelezaji wa uhalifu huo na kutokuwepo kwa fursa ya upatikanaji wa haki , hofu ya unyanyapaa na kukosa huduma kwa manusura ndio vinavyochangia kuripotiwa kwa visa vichache kuliko hali halisi.

Mtoto akicheza nje ya hema katika kambi ya wakimbizi wa ndani mjini Idlib Syria
UNOCHA
Mtoto akicheza nje ya hema katika kambi ya wakimbizi wa ndani mjini Idlib Syria

Ni wakati wa kutoa kipaumbele kwa watoto

Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu katika mizozo ana ujumbe kwa pande zote kinzani katika mizozo “Natoa wito kwa pande zote katika mizozo kutoa kipaumbele mara moja kwa fursa za kibinadamu kuwafikia watoto na watu walio hatarini katika maeneo yenye vita na kuruhusu wataalam wa ulinzi kwa watoto na wahudumu wa misaada ya kibinadamu kufanya kazi yao. Napongeza ujasiri na kujitolea kwa watu haw ana natoa wito kwa nchi wanachama kusaidia kazi ya wataalam wa ulinzi kwa Watoto huko mashinani.”

Ripoti pia imeainisha kwamba muundo wa migogoro mipakani bado unatia hofu ikiwemo eneo la Sahel na bonde la Ziwa Chad.

Ili kushughulikia madhila yanayowakabili watoto hawa, Katibu Mkuu atajumuisha maeneo mengine mawili yanayotia wasiwasi katika ripoti ijayo ambayo ni Burkina Faso na Cameroon.

Hali ya Watoto kushikiliwa kwa madai ya kujihusisha na makundi kinzani katika mzozo ikiwemi uwezekano wa makundi yanayoorodheshwa na Umoja wa Mataifa kama ya kigaidi linasalia kutia wasiwasi kwani jumla ya Watoto 2,500 wanashikiliwa hivi sasa kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Mwakilishi huyo wa Katibu Mkuu anakumbusha kwamba Watoto lazima wachukuliwe kwanza kama waathirika na mahabusu zitumike tu kama suluhisho la mwisho na kwa muda mfupi wakati suluhu mbadala ya mahabusu ikisakwa.

Pia ametoa wito kwa nchi wanachama zinazotia wasiwasi kuwezesha urejeshwaji wa Watoto wa hiyari hasa wale waliokwama katika makambi nchini Iraq na Syria kurudishwa katika nchi zao za asili za wazazi wao.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter