Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tenki za maji Mathare, Nairobi ni lulu katikati ya janga la COVID-19

Hatua za kujizuia maambukizi ya COVID-19 za  zimewekwa katika makazi yasiyokuwa rasmi huko Nairobi, Kenya.
© UNHabitat/Isaac Muasa
Hatua za kujizuia maambukizi ya COVID-19 za zimewekwa katika makazi yasiyokuwa rasmi huko Nairobi, Kenya.

Tenki za maji Mathare, Nairobi ni lulu katikati ya janga la COVID-19

Afya

Maambukizi mapya ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19, yakiendelea kuripotiwa nchini Kenya, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini humo limeanzisha zaidi ya vituo 1000 vya kunawa mikono katika eneo la makazi duni la Mathare kwenye mji mkuu Nairobi, kama njia mojawapo ya kukabiliana na maambukizi mapya.

Eneo la Mathari lina zaidi ya wakazi 200,000 ambao uhaa wa maji safi na salama kwenye eneo hilo ulikuwa ni mwiba katika kutokomeza COVID-19.

Miongoni mwa wakazi wa eneo hilo ni Mary Mwongeli na binti yake Precious Ng’undu mwenye umri wa miaka 9 ambapo Mary anasema kuwa, “baada ya Corona kuathiri masomo, watoto wamerudi nyumbani, na kuna wakati masomo yanafundishwa kupitia televisheni na hivyo huyu mtoto anaketi hapa akiwa makini. “

Precious anasema kuwa “nasoma kwa kutumia televisheni na simu, naandika kwenye daftari, na kile ambacho sielewi namwita mama na kumuomba anifundishe, na ananifundisha.”

Mary anasema kuwa binti yake huandika kwenye daftari na kisha hupeleka shuleni ili mwalimu asahihishe.

Kutokana na janga la Corona, Mary anatoa mafunzo kwa binti yake ambaye anasema, “mama amenieleza kuwa ni lazima kila wakati kunawa mikono yetu, na tusiende kwenye maeneo ya umati kwa kuwa hatufahamu ni nani ana Corona. Na hata wewe mwenyewe hufahamu kama una virusi, na kila wakati unapotoka nje uvae barakoa.”

Akizungumzia vituo vya unawaji mikono huko Mathare, Ally Tifow ambaye ni mtaalamu wa Maji, Huduma za Kujisafi au WASH, UNICEF Kenya anasema kuwa, “huduma hizi ni muhimu katika kuzuia COVID-19, kwa kuzingatia wakazi wa maeneo haya hawana huduma za maji safi na kujisafi. Hapa nchini na hasa vitongoji duni vya mijini kama Nairobi, havina huduma za maji salama.”

Hatua za kujizuia maambukizi ya COVID-19 zimewekwa katika makazi isiyo rasmi huko Nairobi, Kenya.
UN Habitat/Isaac Muasa
Hatua za kujizuia maambukizi ya COVID-19 zimewekwa katika makazi isiyo rasmi huko Nairobi, Kenya.

 

Mary anasema tenki hizo za maji ni msaada mkubwa kwa kuwa, “watu wa UNICEF walikuja wakaleta tenki na kuziweka maeneo ya wazi. Ukitembea tu eneo dogo, unakuta tenki la maji na kuna sabuni, unaweza kunawa mkono na kuondoka.”

Na kwa Precious, yeye ndoto yake ni kuwa daktari ili aweze kuokoa maisha ya watu lakini ujumbe wake ni kwamba, “nataka niwaambie watoto hapo mlipo, lazima mnawe mikono na mvae barakoa.”

Mradi huu wa ufungaji tenki za maji umefanikishwa kwa msaada kutoka shirika la msaada wa kimaendeleo la Uingereza, UK Aid kwa uratibu na serikali ya jiji la Nairobi.