COVID-19: Maandalizi ya kuelekea “kawaida mpya” katika makao makuu ya UN
COVID-19: Maandalizi ya kuelekea “kawaida mpya” katika makao makuu ya UN
"Usalama na afya ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, wawakilishi wa nchi wanachama na wale wote ambao wanatumia jengo letu, ni kipaumbele cha kwanza. Kurejea kwa wafanyakazi jengoni kutazingatia mapendekezo ya jiji na jimbo la New York, ambayo watafuata kadri yatakavyokuja.” Atul Khare, Msaidizi wa Katibu Mkuu katika Operesheni.
Baada ya kurejea katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kufuatia miezi kadhaa ya kufanyia kazi nyumbani kutokana na janga la COVID-19, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, wanadiplomasia, wawakilishi wa mashirika ya kiraia na waandishi wa habari wanaoandikia habari zao kutoka eneo hilo, watalazimika kuzingatia kanuni mpya zilizoandaliwa: mwelekeo wa upande mmoja kwa waendao kwa miguu, lifti kutobeba zaidi ya watu wawili, kuvaa barakoa, na kuketi angalau umbali wa mita 2 kutoka mtu mwingine.
Kwa kuzingatia wa miongozo ya afya ya mamlaka za jiji la New York, makao makuu ya Umoja wa Mataifa bado yamefungwa kwa umma tangu katikati ya mwezi Machi mwaka huu, ni wafanyazi wachache wapatao 100 ndio wanakwenda kazini kwa kuwa wanahitajika kuwepo jengoni. Kadri jiji la New York litakavyolegeza masharti ,vivyo hivyo UN nayo inajiandaa kurejea katika hali ya kawaida, na kurejea huko kutafanyika kwa awamu tatu.
"Usalama na afya ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, wawakilishi wa nchi wanachama na wale wote ambao wanatumia jengo letu, ni kipaumbele cha kwanza. Kurejea kwa wafanyakazi jengoni kutazingatia mapendekezo ya jiji na jimbo la New York, ambayo watafuata kadri yatakavyokuja.” Atul Khare, Msaidizi wa Katibu Mkuu katika Operesheni.
Kwa mujibu wa Idara ya Operesheni na Usaidizi, DOS, mfumo wa kurejea uko katika hatua za mwisho ambapo itaanza awamu ya kwanza. Wafanyakazi wanaohusika na huduma za ufungaji wa mitambo na biashara, FCAS, wanafanya kazi kuandaa ofisi na vyumba vya mikutano.
Tayari kuna vikundi vinafanya kazi kusafisha kwa kutumia dawa za kuuua vidudu maeneo ambayo yako hatarini zaidi na kuna miguso mingi kwenye jengo la makao makuu ya Umoja wa Mataifa. Ikiwemo jengo lenye ghorofa 39 ambalo ni la sekretarieti, ukumbi wa Baraza Ku una majengo ya vyumba vya mikutano na maktaba.
Wafanyakazi hao wanasafisha kwa kina kila wakati maeneo ambayo yanatumika mara kwa mara ikiwemo shoroba, liftin a vyombo bila kusahau samani, vitasa vya milango, swichi za taa, na ngazi.
Wafanyakazi wa DOS wakiweka alama kwenye shoroba na kuta kuonyesha mwelekeo wa watembeo ndani ya jengo ili kuhakikisha iwapo kuna foleni, basi watu wanazingatia umbali wa mita mbili. Vituo vya kutakasa mikono pia vimewekwa kwenye kumbi na maeneo mengine yenye watu wengi, na angalau kituo kimoja cha kutakasa mikono katika kila ghorofa ya ofisi.
Awamu ya 1
Wakati wa awamu ya 1, ni shughuli chache tu zitaruhusiwa. Kwa ujumla jengo halitatakiwa kuwa na watu zaidi ya 400 kwa siku ikilinganishwa na watu 4,200 katika siku za kawaida kabla ya COVID-19. Kwa majengo ya ziada kama vile, DC1 na DC2, idadi ya watu kwa wakati mmoja inatakiwa iwe asilimia 10 ya kiwango cha siku za awali. Lengo ni kuwa na watu wanaotakiwa kuwepo ofisini ili waweze kufanya kazi zao. Shughuli nyingi zitaendelea kufanywa kutokea majumbani.
Wafanyakazi ambao ni lazima wafikie jengoni, ni lazima wavae barakoa lakini hakutakuwepo na ulazima wa kupima joto la mwili ili kuingia jengoni. Vivyo hivyo uchunguzi wa COVDI-19 hautakuwa wa lazima kabla ya kurejea jengoni. Hata hivyo wafanyakazi ambao wanataka kupima virusi vya Corona, wanaweza kuwasiliana na Idara ya Afya na Usalama kazini, DHMOSH, kupitia kurasa maalum. Idara hii inaweza pia kufika nyumbani kwa mfanyakazi ili kupima virusi.
Watu wote ambao watakuwepo jengo la makao makuu, watalazimika kuvaa barakoa pindi wanapita maeneo yenye watu wengi kama vile kumbi, lifti, shoroba, vyooni na njia za kupita watembeao kwa miguu. Hata hivyo, hawatalazimika kuvaa barakoa pindi wanapokuwa kwenye ofisi zao.
Wakati wa awamu ya 1 na 2 ya kurejea, mikutano ya uso kwa uso, iwe ya kiutawala au ya shirika haitaruhusiwa.
Kuanza awamu ya 1, ni lazima amri iliyotangazwa na New York, ilegezwe..
Awamu ya 2
Wakati wa awamu ya 2, idadi ya watu kwenye jengo la makao makuu litaongezwa taratibu hadi kuwa 1,100 kwa siku, sawa na asilimia 40 hadi 50 ya viwango vya kabla ya COVID-19. Wafanyakazi wengine wataendelea kufanyika kazi nyumbani. Kutoka awamu 1 kwenda ya 2, kutahitaji kupungua zaidi kwa maambukizi na kuimarishwa kwa mifumo ya afya ya jiji mwenyeji.
Awamu ya 3 - "Kawaida mpya"
Kipindi cha mpito kuelekea awamu ya 3 – kikijulikana kama “ukawaida mpya” – kitafanyika pindi hatari za maambukizi kazini zitakapokuwa zimepunguzwa kutoka kipindi cha kabla ya janga kuanza na vikwazo kuhusiana na COVID-19 viwe vimeondolewa na jiji na jimbo la New York., hususan vile vinavyohusu malezi ya watoto na shule za umma. DOS inazingatia kuwa bado ni mapema sana kuainisha kanuni za kazi wakati wa awamu hii ya 3.
Mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Muundo wa mjadala mkuu wa mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, uliopangwa kufanyika mwezi Septemba, kwenye makao makuu wakati wa mkutano wa 75 wa Baraza Kuu, sambamba na mikutano mingine ya ngazi ya juu, unaweza kubadilika.
Katika barua yake kwa Rais wa Baraza Kuu, Tijjani Muhammad-Bande, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, alipendekeza kuwa Baraza Kuu lifanye mjadala wake kwa mfumo tofauti. Mathalani, linaweza kutumia ujumbe uliorekodiwa awali kutoka kwa wakuu wa nchi na serikali au mawaziri, na kupunguza idadi ya watu watakaokuwepo kwenye ukumbi wa Baraza Kuu kuwa mwakilishi mmoja kwa kila ubalozi wenye makao yake New York.
"COVID-19 imebadili jinsi tunavyoishi na tunavyoshirikiana,” amesema msaidizi wa Katibu Mkuu, Atul Khare, akiongeza kuwa, “lakini tuna mnepo na pamoja tunaweza kushinda hili, huku tukiheshimu, bila shaka umbali wa kutogusana.”
Taarifa kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa: kadri janga linavyozidi kubadilika wiki zijazo, taarifa kuhusu mpango wa kurejea awamu ya 3 zitakuwa zinaongezwa kwenye ukurasa wa “afya na usalama wa kitengo cha menejimenti ya majanga na kuchapishwa kwenye Pahala Petu pa Kazi, wavuti ya Iseek.