Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ingawa dunia ina chakula cha ziada watu milioni 830 wanakabiliwa na njaa:UN

Mwanamke akibeba magunia ya mbegu zilizosambazwa kwa familia huko Sudani Kusini wakati wa janga la COVID-19.
FAO/Mayak Akuot
Mwanamke akibeba magunia ya mbegu zilizosambazwa kwa familia huko Sudani Kusini wakati wa janga la COVID-19.

Ingawa dunia ina chakula cha ziada watu milioni 830 wanakabiliwa na njaa:UN

Msaada wa Kibinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema dunia ina chakula cha kutosha kulisha watu wote na ziada lakini cha kusikitisha ni kwamba watu zaidi ya milioni 800 wanakabiliwa na njaa. 

 

Bwana Guterres ameyasema hayo leo kupitia ujumbe maalum wa uzinduzi wa sera kuhusu uhakika wa chakula uliofanyika kwa njia ya mtandao na kusema kuwa kuna zaidi ya chakula cha kutosha ulimwenguni kulisha idadi yote ya watu bilioni 7.8 lakini “Leo hii, zaidi ya watu milioni 820 wana njaa. Na watoto wapatao milioni 144 wa chini ya umri wa miaka 5 wamedumaa , ikiwa ni zaidi ya mtoto mmoja kati ya watoto watano duniani. Mifumo yetu ya chakula inashindwa, na janga la Covid-19 linafanya mambo kuwa mabaya zaidi.”

Ameonya kwamba endapo hatua za haraka hazitachukuliwa, ni dhahiri kwamba kuna dharura ya chakula ulimwenguni ambayo inaweza kuwa na athari za muda mrefu kwa mamia ya mamilioni ya watoto na watu wazima.

Watu zaidi kuingia katika umasikini

Ameongeza kuwa“Mwaka huu, watu milioni 49 zaidi wanaweza kutumbukia katika umaskini uliokithiri kwa sababu ya janga la Covid-19. Idadi ya watu watakao kuwa na upungufu wa chakula au ukosefu wa lishe bora itaongezeka haraka. Na kila kiwango cha asilimia kinachoshuka katika jumla ya pato la taifa inamaanisha watoto milioni 0.7 zaidi watadumaa.”

Katibu Mkuu amesema hata katika nchi zenye chakula kingi kunashuhudiwa hatari za usumbufu katika mnyororo wa usambazaji wa chakula. Amesisitiza kwamba kunahitajika kuchukuliwa hatua sasa ili kuepusha athari mbaya zaidi za juhudi za kudhibiti ugonjwa huu wa corona.

Guterres amesem leo  anazindua mpango wa sera wa athari za COVID-19 katika uhakika wa chakula na lishe. Ambayo ina matokeo matatu ya wazi.

Mambo matatu muhimu

Kwanza, lazima kuhamasisha kuokoa maisha na uhai, kwa kuzingatia umakini ambapo hatari ni kubwa sana. Hiyo inamaanisha kubuni huduma za chakula na lishe kama ni muhimu, wakati wa kutekeleza kinga zinazofaa kwa wafanyakazi wa chakula. 

Inamaanisha kuhifadhi chakula muhimu cha kibinadamu, utu na msaada wa lishe kwa watu walio hatarini. Na inamaanisha kutoa chakula katika nchi zenye shida ya chakula ili kuimarisha na kuongeza mifumo ya kuilinda jamii.

Nchi zinahitajika kuongeza msaada katika usindikaji wa vyakula, usafirishaji na masoko ya chakula ya ndani, na lazima ziweke maeneo ya  biashara wazi ili kuhakikisha utendaji kazi endelevu wa mifumo ya chakula.

Chakula tunacho cha kutosha mamilioni wahaha na njaa:UN

"Na ni lazima tuhakikishe kwamba vifurushi vya misaada vinawafikia walio hatarini zaidi, pamoja na kukidhi mahitaji ya ukwasi wa wazalishaji wadogo wa chakula na biashara za vijijini."

Pili, lazima kuimarisha mifumo ya kuilinda jamii kwa lishe. Nchi zinahitaji kulinda upatikanaji wa lishe salama, hususani kwa watoto wadogo, wanawake wajawazito na na wanaonyoyesha, wazee na makundi mengine yaliyo hatarini.

Na zinanahitaji kuridhia na kuendeleza miradi ya kuilinda jamii ili kunufaisha makundi yenye uhitaji wa lishe yaliyo kwenye hatari. Guterres amesema hii ni pamoja na kusaidia watoto ambao  hawawezi tena kupata mlo shuleni.

Tatu, lazima tuwekeze kwa ajili ya baadaye. Ameongeza kuwa dunia ina jukumu la kujenga jamii jumuishi na endelevu.

“Tujenge mifumo ya chakula inayoshughulikia vyema mahitaji ya wazalishaji wa chakula na wafanyakazi. Tutoe ufikiaji unaojumuisha zaidi  chakula, afya na lishe ili tuweze kutokomeza njaa. Na turekebishe uhusiano kati ya mifumo ya chakula na mazingira asilia kwa kuzibadilisha zifanye kazi vizuri  kwa asilia na kwa ajili ya hali ya hewa.”

Na biila kusahau kwamba mifumo ya chakula inachamgia hadi asilimia 29 ya uzalishaji wote wa gesi chafu, ikijumuisha asilimia 44 ya methane, na zina athari mbaya kwa bayoanuai.

Amehitimisha akisema “endapo tutafanya mambo haya na zaidi, kama tunavyozindia leo, tunaweza kuzuia athari mbaya zaidi za janga la COVID-19 katika uhakika wa chakula na lishe na tunaweza kufanya hivyo kwa njia inayounga mkono mabadiliko ynayojali mazingira ambayo tunahitaji kuyatengeneza.”