Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabaharia zaidi ya 150,000 wakwama melini sababu ya COVID-19:ILO

Meli zikiwa katika bandari ya Antwerp
Picha/ IMO
Meli zikiwa katika bandari ya Antwerp

Mabaharia zaidi ya 150,000 wakwama melini sababu ya COVID-19:ILO

Afya

Mabaharia wanapaswa kuchukuliwa kama wafanyakazi muhimu hivyo wanastahili kuruhusiwa kurejea nyumbani -limesema leo shirika la kazi duniani ILO, wakati likitoa wito wa hatua za haraka za kuwaachilia mabaharia  kati ya 150,000 hadi 200,000 waliokwama kwenye meli kote duniani kwa sababu ya hatua za kukabiliana na janga la virusi vya corona au COVID-19.

ILO imezitaka mamlaka za serikali, uhamiaji, afya na masuala ya bahari kushirikiana kutambua kwamba mabaharia ni wafanyakazi muhimu ambao wanahakikisha kuendelea kwa biashara na usafirishwaji wa madawa muhimu, vifaa vya usalama, chkula na bidha nyingine muhimu wakati wa janga hili la corona.

Likirejelea mkataba wa ajira za usafiri wa bahari wa mwaka 2006, shirika hilo la ILO limetoa wito kwa serikali kupitisha haraka bila kuchelewa hatua zozote zinazowezekana kuwezesha mabadiliko ya wahudumu wa melini na kuwasafirisha mabaharia huku hatua zote muhimu zikichukuliwa kupunguza hatari ya maambukizi.

Zaidi y mwezi mmoja baada ya ILO kutoa onyo mwishoni mwa mwezi Aprili kuhusu mgogoro wa kuwakatalia ruhusu mabaharia kuondoka katika meli zao, kumekuwa na maendeleo kidogo sana yaliyofikiwa na kwa mujibu wa ILO hali inazidi kuwa mbaya kila uchao.

Asilimia kuwa ya mabaharia hao waliokwama melini wengi wamemaliza ziara zao za kazi zaidi ya miezi minne iliyopita lakini wakati mikataba imeongezwa zaidi sababi ya janga la corona wengi wao sasa wanaripotiwa kusumbuliwa na matatizo ya akili na uchovu hali ambayo inapunguza uwezo wao wa kufanyakazi.

“Kuwalazimisha mabaharia waliochoka kuendelea kufanyakazi zaidi ya miezi minne baada ya mikataba yao kwisha haikubaliki.Hali hii inaweka hatarini afya zao na kuhatarisha usalama na bahari, tunatoa wito kwa serikali kufanyakazi pamoja kuhkikisha mabaharia hawa wanabadilishwa kwa njia salama.” Amesema Guy Ryder mkurugenzi mkuu wa ILO.

Ameongeza kuwa wakati huohuo vikwazo vya kubadilisha mabaharia vilivyowekwa na nchi kwa ajili ya kupunguza kusambaa kwa maambukizi ya COVID-19 kumemaanisha kwamba mabaharia wanaosubiri kurejea tena baharini wamepoteza vipato.

“Nawaomba nchi wanachama kutambua mabaharia kama wafanyakazi muhimu na kuchukua hatua za haraka zinazohitajika ambazo zinawawezesha ambao wamekuwa wakifanyakazi kwa bidii kuendelea kutupatia madawa , chakula na bidhaa nyingine za muhimu kwenda nyumbani na kubadilishwa na mabaharia wengine ambao waki fiti na wenye nguvu.”

Wito wa kutaka mabaharia kuchukuliwa kama wafanyakazi wa muhimu sana uliwekwa kwenye taarifa ya pamoj iliyoyolewa Mei 22 na shirika la kimataifa la usafiri wa anga ICAO, shirika la kimataifa la usafiri wa majini IMO na shirika la ILO. Wito huu utawaepusha mabaharia na vikwazo vya kusafiri na kuwezesha kuondoka au kuingia melini pasi shaka.