Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 9 za kimarekani kutoka tumbaku zinatumika kuwavutia vijana kujaza nafasi ya wanaouawa na bidhaa hiyo kila mwaka-WHO

WHO inatoa wito kwa vijana wote kuungana kupigana na Tumbaku ili kuwa kizazi kisicho tumia tumbaku.
WHO
WHO inatoa wito kwa vijana wote kuungana kupigana na Tumbaku ili kuwa kizazi kisicho tumia tumbaku.

Dola bilioni 9 za kimarekani kutoka tumbaku zinatumika kuwavutia vijana kujaza nafasi ya wanaouawa na bidhaa hiyo kila mwaka-WHO

Afya

Ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kimataifa ya kutovuta tumbaku, siku inayoadhimishwa kila tarehe 31 mwezi Mei ili kukuza uelewa kuhusu madhara ya zao hilo, shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO linaeleza kuwa kila mwaka tasnia ya tumbaku inawekeza zaidi ya dola bilioni 9 za kimarekani kutangaza bidhaa zake zaidi ikiwalenga vijana na nikotini na tumbaku kwa nia ya kujaza nafasi ya watu milioni 8 ambao bidhaa hiyo inawaua kila mwaka.

WHO inasema kutokana na hali hiyo, “zaidi ya vijana wadogo milioni 40 wa umri kati ya mika 13 na 15 tayari wameanza kutumia tumbaku.”

Ili kuwafikia vijana, shirika hilo la afya la Umoja wa Mataifa limezindua shindano lililopewa kitambulisho cha #TobaccoExposed yaani #TumbakuImeumbuliwa katika mtandao wa TikTok na kuwakaribisha wadau wa mitandao ya kijamii kama Pinterest, Youtube na Tiktok kuusambaza ujumbe.

Wakati huo huo WHO imetoa wito kwa sekta zote kuacha kutangaza mbinu za tumbaku na viwanda vingine vinavyohusika katika kuwawinda watoto na vijana wa umri mdogo.

Aidha WHO imetoa ushauri kwa makundi mbalimbali katika jamii kuwaokoa watoto na janga la tumbaku ambapo kwa shule zimeshauriwa zikatae aina yoyote ya udhamini na zizuie wawakilishi wa makampuni ya nikoyini na tumbaku kuzungumza na wanafunzi.

Sigara ya  kielektroniki
WHO
Sigara ya kielektroniki

 

Watu maarufu na wenye ushawishi wakatae udhamini wowote unaotoka katika makapmuni ya tumbaku, Televisheni na huduma za kurusha maudhui mitandaoni ziache kuonesha tumbaku na sigara za kielektroniki, mitandao ya kijamii ipige marufuku kutangazwa kwa tumbaku na bidhaa nyingine zinazohusina na bidhaa za tumbaku, serikali na sekta za kifedha ziachane na viwanda vya tumbaku na vingine vinavyohusiana navyo na pia serikali zipige marufuku aina zote za matangazo, promosheni na udhamini wa tumbaku.

“Nchi zinaweza kuwalinda watoto dhidi ya unyonyaji wa tasinia hii ya tumbaku kwa kuweka sheria kali dhidi ya tumbaku zikiwemo bidhaa za sugara za kielektoniki ambazo tayari zimeanza kuteka kizazi kipya cha vijana wadogo.” Imeshauri WHO.