Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wawili kati ya waliosafiri na ndege maalum ya UNAMID kutoka El Fasher,Sudan wakutwa na COVID-19 Nairobi

Polisi wa UNAMID wakiwezesha mafunzo ya lugha ya kiingereza kwa wanawake wakimbizi wa ndani mjini El Fasher , Kaskazini mwa Darfur Sudan
UN Photo/Albert Gonzalez Farran
Polisi wa UNAMID wakiwezesha mafunzo ya lugha ya kiingereza kwa wanawake wakimbizi wa ndani mjini El Fasher , Kaskazini mwa Darfur Sudan

Wawili kati ya waliosafiri na ndege maalum ya UNAMID kutoka El Fasher,Sudan wakutwa na COVID-19 Nairobi

Afya

Ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika huko Darfur, Sudan, UNAMID umetangaza kuwa unashirikiana na mamlaka nchini Kenya kuwahudumia maafisa waliokutwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Taarifa ya UNAMID, iliyotolewa hii leo mjini Khartoum imesema, “UNAMID inasikitika kutangaza kuwa abiria wawili waliosafiri na ndege maalum ya UNAMID kutoka kituo chake cha El Fasher kwenda jijini Nairobi Kenya juzi tatehe 27 mwezi huu wa Mei, wamekutwa na virusi vya corona au ugonjwa wa coronavirus">COVID-19 walipopimwa na mamlaka za afya za Kenya mara tu walipofika katika Uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta.”

Ndege hiyo ilikuwa imewabeba maafisa tofautitofauti kutoka UNAMID, ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini humo, UNCT na kutoka shirika la kiserikali, pia maafisa wa UNAMID ambao walikuwa wamajitolea kuondoka kutokana na kuwa wana hali ya afya ambayo inawaweka hatarini zaidi ikiwa wangepata maambukizi ya virusi vya corona katika mazingira ya kazi.

Abiria wawili walitambuliwa kuwa na maambukizi ya COVID-19 walipowasili Nairobi na wakati wakifanyiwa uchunguzi. Mmoja wa wagonjwa hao ni afisa wa UNAMID na mwingine ni mwajiriwa wa shirika lisilo la serikali ambalo linafanya kazi zake Darful kwa kushirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa.

“Hakuna abiria yeyote aliyeonesha kuwa na dalili za kawaida za virusi vya corona au maambukizoi mengine yoyote wakati walipokuwa wakikaguliwa kabla ya safari.” Imeeleza taarifa hiyo.

UNAMID inashirikiana kwa ukaribu na mamlaka za Kenya jijini Nairobi kuhakikisha mfanyakazi wake aliyeathirika anapata huduma ya matibabu iliyopo. Abiria wengine waliokuwa katika ndege hiyo maalumu wamewekwa karantini na wako katika uangalizi wa kitabibu kwa mujibu wa taratibu za kushughulikia ugonjwa wa COVID-19 nchini Kenya. UNAMID imeanzisha ufuatiliaji wa watu wote waliokutana na watu waliokuwa katika ndege hiyo na inapitia upya taratibu za jumla kuhusiana na safari za wafanyakazoi wake.