Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yazindua zana ya kuwaelimisha wanafunzi dhidi ya kuingia katika matumizi ya tumbaku

Tumbaku inaua watu millioni 8 kila mwaka-WHO
Unsplash/Sebastiaan Stam
Tumbaku inaua watu millioni 8 kila mwaka-WHO

WHO yazindua zana ya kuwaelimisha wanafunzi dhidi ya kuingia katika matumizi ya tumbaku

Afya

Kuelekea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kutovuta tumbaku, keshokutwa Jumapili, shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO hii leo Ijumaa linazindua mwongozo au zana mpya kwa ajili ya wanafunzi wa umri wa kuanzia miaka 13 hadi 17 kuwatahadharisha na mbinu za tasnia ya tumbaku zinazotumika kuwavutia na bidhaa hiyo yenye kuleta uraibu.

Kampeni ya mwaka huu ya siku ya kimataifa ya kutotumia bidhaa za tumbaku inajikita katika kuwalinda watoto na vijana dhidi ya unyonyaji unaofanywa na makampuni ya tumbaku na mengine yenye uhusiano na hayo. Zana hiyo ya mwongozo inayozinduliwa ina masula ya shughuli za darasani ikiwemo inayowaweka wanafunzi katika uelewa wa kina kuhusu tasnia ya tumbaku ili kuwafanya waelewe tasnia hiyo inavyojaribu kuwadanganya kuingia katika bidhaa hizo hatari. Zana hizo ni pamoja na video za kuelimisha, maswali ya chemsha bongo na kazi za nyumbani.

Zana hiyo inafichua mbinu kama vile matamasha yanayoandaliwa na makampuni ya tumbaku au makampuni mengine yanayohusiana na hayo, sigara za kielektroniki zilizotiwa ladha mbalimbali ambazo zinawavutia vijana, wawakilishi wa sigara hizo kuja kutoa maelezo katika shule, na pia bidhaa kuoneshwa katika vipindi mbalimbali vya vijana.

Taarifa ya WHO imesema kuwa hata wakati huu wa janga la COVID-19, tasnia ya tumbaku na nikotini bado inaendelea kusukuma bidhaa ambazo zinawabana au kuwapunguzuia watu  uwezo wa kupambana na virusi vya corona na kupona dhidi ya ugonjwa huo.

"Tasnia ya tumbaku imetoa barakoa za bure zenye nembo za bidhaa hizo na wanajitolea kukuletea bidhaa mlangoni kwako wakati wa karantini na wameshawishi bidhaa zao ziwekwe katika orodha ya bidhaa muhimu.” Imeeleza WHO.

Uvutaji wa tumbaku unayanyima hewa mapafu na viungo vingine kwa kuvinyima hewa ya oksijeni ambayo viungo hivyo vinaihitaji ili kufanya kazi sawasawa. Mkurugenzi wa uhamasishaji wa afya katika WHO, Ruediger Krech, “kuwaelimisha vijana ni muhimu kwa sababu takribani wavutaji 9 kati ya 10 wanaanza kabla ya kutimiza umri wa miaka 18. Tunataka kuwapatia vijana wadogo ufahamu wa kukataa udanganyifu wa tasnia ya tumbaku.”