Mtoto kiziwi alazimika kuosha magari jijini Kinshasa ili alee familia yake

26 Mei 2020

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, athari za janga la virusi vya Corona au COVID-19 zimekuwa mbayá zaidi kwa watoto wenye ulemavu, ambapo mtoto mmoja mkazi wa mji mkuu Kinshasa, ambaye ni kiziwi, amelazimika kusaka mbinu za kuweza kupata kipato ili kusaidia familia yake.

Mtoto huyo, Steve Okito mwenye umri wa miaka 14, anaishi jijini kinshasa na mama yake na wadogo zake watatu wa kiume. Yeye ni mwanafunzi wa darasa la 7, lakini sasa hawezi tena kwenda shule.

Katika mfululizo wa video za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF zinazolenga kupaza sauti za vijana, Steve anaonekana akizungumza kwa lugha ya alama na anasema kuwa “shule zimefungwa kwa sababu ya janga la virusi vya Corona. Siwezi tena kuwaona marafiki zangu.”

Mtoto huyu anatoka familia maskini, na mama yake amepooza kwa hiyo analazimika kusaka kazi na kile afanyacho ni kusafisha magari jijini Kinshasa ili apate ujira.

Steve anasema kuwa, “sasa hivi naosha magari kwa sababu shule imefungwa. Kila kitu kimefungwa na ninalazimika kupata fedha ili nisaidie familia yangu. Fedha nampatia mama yangu. Hapa kwa mfano nimeosha hili gari na nimepata faranga 3000 sawa na dola 2. Lakini inategemea na mmiliki, wakati mwingine naweza kupata malipo ya juu zaidi.”

Ujio wa janga la Corona umefanya maisha ya Steve kuwa magumu zaidi kwa sababu hali ni ngumu zaidi kwa yeye kupata fedha akisema kuwa, “kabla ya Corona, magari ya kuosha yalikuwa ni mengi, lakini sasa kila kitu kimefungwa, hakuna mtu anayewasha gari kwenda kutembelea rafiki au kuzunguka tu.”

Matarajio ya Steve ni kuwa shule zitafunguliwa ili aweze kuwaona tena rafiki zake,   shule zimefungwa kwa sababu ya COVID-19.

Hata hivyo Wizara ya afya ya DRC, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na wadau wanaendelea kushirikiana ili kuwepo kwa wafanyakazi wa kuwapatia watoto kama Steve msaada wa kisaikolojia ili waweze kuhimili madhara ya muda mfupi na muda mrefu ya janga la COVID-19.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter