Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamishna wa haki za binadamu akaribisha kukamatwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda

Wakimbizi wa Rwanda ambao waliikimbia nchi wakati wa mauaji ya kimbari, katika picha walipokuwa wakirejea nyumbani.
UN Photo/John Isaac
Wakimbizi wa Rwanda ambao waliikimbia nchi wakati wa mauaji ya kimbari, katika picha walipokuwa wakirejea nyumbani.

Kamishna wa haki za binadamu akaribisha kukamatwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet hii leo mjini Geneva Uswisi amekaribisha kukamatwa kwa  Felicien Kabuga ambaye anatuhumiwa kuongoza mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi nchini Rwanda yalitotekelezwa mwana 1994.

Bi Bachelet amesema, “kukamatwa kwa Félicien Kabuga, miaka 26 baada ya mauaji ya kimbari, kunasisitiza ufikiaji mrefu wa uwajibikaji kwa makosa ya kimataifa. Hakuna ambaye anafanya makosa ya kimataifa anatakiwa kufikiri kuwa kupita kwa wakati wanaweza kukwepa mkono wa haki na kwamba hawatawajibishwa.”

Kabuga alikuwa ameshtumiwa mnamo mwaka 1997 na Mahakama ya Makosa ya Jinai ya Rwanda (ICTR) kwa makosa saba  ikiwa ni pamoja na mauaji ya kimbari, ushiriki katika mauaji ya kimbari, na pia uchochezi wa moja kwa moja na wa umma wa kutekeleza mauaji ya kimbari - yote haya yakiwa na uhusiano na uhalifu uliofanywa dhidi ya watutsi nchini Rwanda.

Félicien Kabuga, mmoja wa watoro wa hali ya juu duniani anatuhumiwa kuwa kinara wa mauaji ya Rwanda amekamatwa leo 16 Mei 2020 mjini Paris, Ufaransa.
IRMCT Video
Félicien Kabuga, mmoja wa watoro wa hali ya juu duniani anatuhumiwa kuwa kinara wa mauaji ya Rwanda amekamatwa leo 16 Mei 2020 mjini Paris, Ufaransa.

 

Kwa mujibu wa shutuma, Kabuga pamoja na wengine, wanatuhumiwa kutumia Kituo cha redio cha Radio Television Libre des Mille Collines (RTLM) kuchochea zaidi chuki kati ya watu wa kabila la wahutu na watutsi nchini Rwanda. 

Kabuga pia anatuhumiwa yeye pamoja na wengine, kuanzisha uchangishaji fedha za kufadhili kundi la wanamgambo wa Interahamwe ambalo liliongoza mauaji dhidi ya watutsi, katika kipindi ambacho watu wa kabila la wahutu ambao waliyapinga mauaji, nao waliuawa.

 “Tunapoendelea hii leo kuona hatari ya habar iza uongo, chuki ya rangi na ukabila na uchochezi wa vurugu vikisambazwa kwa ukubwa, kesi ya Kabuga na matokeo ya propaganda yaliyotangazwa na Radio Television Libre des Mille Collines, ni ukumbusho wa lugha kama hiyo inakoweza kutupeleka, nani kwa nini kupambana navyo ni muhimu.” Amesema Bi Bachelet. 

Aidha Bi Bachelet amepongeza ueledi wa mwendesha mashitaka Serge Brammertz na timu yake pamoja na mamlaka za Ufaransa, na juhudi za mamlaka za kutekeleza sheria katika nchi nyingine ambao kwa pamoja walifanikisha kukamatwa kwa Kabuga nchini Ufaransa mwezi huu wa Mei, tarehe 16.