Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtuhumiwa kinara wa mauaji ya kimbari Rwanda anaswa Ufaransa, UN yapongeza

Félicien Kabuga, mmoja wa watoro wa hali ya juu duniani anatuhumiwa kuwa kinara wa mauaji ya Rwanda amekamatwa leo 16 Mei 2020 mjini Paris, Ufaransa.
IRMCT Video
Félicien Kabuga, mmoja wa watoro wa hali ya juu duniani anatuhumiwa kuwa kinara wa mauaji ya Rwanda amekamatwa leo 16 Mei 2020 mjini Paris, Ufaransa.

Mtuhumiwa kinara wa mauaji ya kimbari Rwanda anaswa Ufaransa, UN yapongeza

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Hatimaye mtuhumiwa kinara wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda Félicien Kabuga amekamatwa hii leo mjini Paris nchini Ufaransa.
 

Kabuga, amekamatwa kufuatia uchunguzi wa pamoja na ofisi ya mwendesha mashtaka ya mfumo wa kimataifa wa kushughulikia mabaki ya kesi za mauaji ya kimbari, IRMCT.

Kufuatia taarifa za kukamatwa kwa Kabuga, mwendesha mashtaka mkuu wa IRMCT Serge Brammertz ametoa taarifa yake kutoka jijini Arusha, nchini Tanzania na The Hague, Uholanzi, akisema kuwa, “kukamatwa kwa Félicien Kabuga ni kumbusho ya kwamba wahusika wote wa mauaji ya kimbari wanaweza kuwajibishwa hata baada ya miaka 26 ya kutekeleza uovu wao.”

Amesema fikra zao ni kwa wahanga na manusura wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda na kwamba “wakumbuke ofisi yangu inawatetea kwa ueledi mkubwa.”

Bwana Brammertz amesema kwa upande wa haki za kimataifa, kukamatwa kwa Kabuga kunadhihirisha “tunaweza kufanikiwa pindi kuna usaidizi wa kimataifa. Matokeo haya ni mchango wa msaada usiotetereka kutoka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo lilianzisha mfumo huu wa kuendeleza mchakato wa kuwajibisha wahusika wa masuala ya Rwanda na iliyokuwa Yugoslavia.”

Mwendesha mashtaka huyo mkuu wa IRMCT ametoa shukrani zake za dhati kwa Ufaransa na mamlaka za usimamizi wa sheria hususan ofisi kuu ya kutokomeza uhalifu dhidi ya binadamu, mauaji ya kimbari na uhalifu wa kivita, akisema kuwa kukamatwa kwa mtoro huyo kusingalifanikiwa bila ushirikiano na stadi zao.

Baada ya kukamilishwa kwa taratibu kwa mujibu wa sheria za Ufaransa, Kabuga atahamishiwa katika eneo lililo chini ya IRMCT ambako kesi yake itaanza kusikilizwa.

Hata baada ya robo karne utakamatwa tu; Guterres

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha kitendo cha kukamatwa hii leo kwa Kabuga ambaye amekuwa akisakwa tangu mwaka 2013.

Bwana Guterres kupitia taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na msemaji wake, amesema kuwa "kukamatwa kwa Kabuga kunatuma ujumbe mzito ya kwamba wale wanaotuhumiwa kufanya uhalifu kama unaomkabili hawawezi kukwepa sheria na kwamba mwishowe watawajibishwa hata ikiwa ni baada ya robo karne."

Amepongeza ushirikiano kati ya IRMCT na mamlaka za Ufaransa na ametoa wito kwa serikali kuendelea kushirikiana ili kukamata, kuwatia korokoroni, kuwakabisha na kuwapeleka maeneo husika wengine wote ambao bado wanaskwa kwa uhalifu huo.

Katibu Mkuu amesema fikra zake zinasalia na wahanga na manusura wa vitendo vinavyodaiwa kutekelezwa na Kabuga akiongeza kuwa kukomesha ukwepaji sheria ni muhimu kwa ajili ya amani, usalama na haki.

Kabuga alishtakiwa na mahakama ya Umoja wa Mataifa ya uhalifu wa Rwanda mwaka 1997 kwa makosa 7 ya mauaji ya kimbari, kushiriki mauaji, kuelekeza na kuchochea umma kufanya mauaji, kupanga mauaji, kutesa na kuua, yote hayo yakihusishwa na uhalifu uliotekelezwa wakati wa mauaij ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994 dhidi ya watutsi.

Félicien Kabuga alikuwa Rais wa chama cha Comité Provisoire of the Fonds de défense nationale kwa kipindi cha miaka 25 kilichokomea mwezi Julai mwaka 1994.

Halikadhalika alikuwa rais wa Comité d’Initiative of Radio Television Libre des Milles Collines kwa kifupi, RTLM, katika kipindi ambacho anadaiwa kutenda makosa 7 aliyoshtakiwa nayo.