UN yakusanya msaada, mgonjwa wa kwanza wa COVID-19 akibainika makambi ya Rohingya

Mjini Geneva UswisI msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Andrej Mahecic ametangaza thibitisho la serikali kwamba mmoja wa wakimbizi wa Rohingya amepimwa na kupatikana na virusi vya corona katika makazi ya Katupalong Cox’s Bazar, Pamoja na raia mwingine kutoka katika jamii inayowahifadhi ya Bangladesh.
“Kuna hofu kubwa kuhusu uwezekano wa athari kubwa za virusi hivyo kwenye makazi ya wakimbizi yaliyofurika, yanayohifadhi wakimbizi wa Rohigya 860,000. Watu wengine 400,000 raia wa Bangladesh wanaishi kwenye maeneo jirani kama jamii zinazowahifadhi wakimbizi hao. Watu hawa wanachukuliwa kuwa ni miongoni mwa walio katika hatari zaidi duniani dhidi ya janga hili.”
Mashirika ya Umoja wa Mataifa tayari yameweka mipango ya dharura ya kukabiliana na COVID-19 kwenye makazi ya Cox’s Bazar likiwemo shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM, yametenga maeneo maalum 35 ya kutoa huduma pamoja na maeneo matatu ya kutenga wagonjwa na kuwapa matibabu.
Pia mashirika hayo yanakaribia kukamilisha kituo cha kuarantini ambacho kina ukubwa wa kuweka watu 465 na vitanda 250 ya wagonjwa mahututi wa corona.
Ingawa kuwasili kwa ugonjwa huo kambini kulitarajiwa kunaongeza shinikizo kwa watu hao ambao wako hatarini hasa sasa wakijiandaa na msimu wa mvua za monsoon ambazo zinakaribia.
Mwezi Agosti mwaka huu itakuwa ni miaka mitatu tangu wakimbizi wa Rohingya walio Cox’s Bazar Bangladesh walipofungasha virago na kukimbia machafuko, mateso na mauaji kwenye jimbo la Rakhine katika nchi jirani ya Myanmar.
Mwaka jana watu 16,000 waliathirika vibaya na mvua kubwa zilizonyesha kwa muda was aa 24.
Ili kusaidia shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP linahaha kusafisha mitaro na maeneo ya mwinuko ambayo yanauwezekano mkubwa wa kuathirika na mvua kubwa itakayonyesha.
Shirika hilo limeonya kwamba COVID-19 inatishia kugeuza mafanikio yaliyopatikana nchini Bangladesh kwa miaka 50 iliyopita na linaomba dola milioni 320 ili kuwasaidia watu wasiojiweza na walio katika hatari zaidi.
Dola milioni 320 zahitajika kwa Warohingya na jamii zinazowahifadhi
Kwa mujibu wa shirika hilo dola milioni 200 kati ya fedha hizi zinahitajika kwa ajili ya hatua za kupambana na COVID-19 nchini Bangladesh na zinazosalia milioni 120 zinahitajika kusaidia hasa Waislam wa kabila la Rohingya katika miezi sita ijayo.
“Watu kutakiwa kusalia majumbani na vikwazo vya kutembea vinaathiri Maisha ya mamilioni ya wabangladesh hususan wanaotegemea kipato cha siku kama vile madereva, na vibarua ambao ambao sasa wanajikuta hawawezi kukidhi mahitaji ya msingi " Amesema Elizabeth Byrs msemaji wa WFP.
Chini ya mpango wa WFP fedha hizo za ufadhili zitahakikisha uhakika wa chakula kwa familia kwenye maeneo ya vijijini na mitaa ya mabanda mijini na pia kwa viabarua wanaolipwa wa siku.
Na kwa wakati huu shirika hilo la WFP limehakikisha kuendelea kwa mgao wa kitaifa wa mchele, fedha taslim na mipango ya lishe kwa ajili ya kusaidia msaada unaotolewa na serikali.
Pia WFP imeanza kujenga maghala ya kuhifadhi chakula na vitu visivyo chakula ambavyo ni vya lazima katika vita dhidi ya COVID-19 ikiwemo vifaa vya kujikinga na inasaidia mashirika mengine ya misaada kwa kusambaza misaada na bidhaa nyingine ndani ya Bangladesh.