Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mialo ya ziwa Victoria imejaa maji, mama lishe Mwanza wapaza sauti

Wavuvi kutoka Kenya wakiwa katika harakati za uvuvi kwenye ziwa Victoria ambako Sangara ndiko makazi yake zaidi
FAO/Ami Vitale
Wavuvi kutoka Kenya wakiwa katika harakati za uvuvi kwenye ziwa Victoria ambako Sangara ndiko makazi yake zaidi

Mialo ya ziwa Victoria imejaa maji, mama lishe Mwanza wapaza sauti

Tabianchi na mazingira

Ripoti za  kuendelea kuongezeka kwa kina cha maji katika Ziwa Viktoria barani Afrika zimeendelea kuenea na sasa waathirika wa hali hiyo wanazungumza kupaza sauti zao ili waweze kupatiwa msaada wakati huu ambapo njia zao za kujipatia kipato zimeathiriwa na ongezeko la kiwango cha maji.

 

Rose ni miongoni mwa wakazi wa maeneo haya pembezoni mwa ziwa viktoria Mwanza Nchini Tanzania, Ziwa hili ambalo ni kubwa zaidi barani Afrika linatumiwa na Kenya, Uganda na Tanzania, likiwa ni makaazi, sehemu za biashara, kama mialo na sehemu za kupumzika na biashara ndogondogo. Hata hivyo kutokana mabadiliko  ya tabianchi  hali ni tofauti.

Kwa sasa ziwa hili limejaa maji kupita kiasi na kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi kandokando mwa ziwa hili kama anavyoeleza Rose akisema kuwa, "ndio hivyo maji  yamekuwa mengi sana.Tumeathirika kwa kweli  mpaka wengine wameamua kufunga vibanda kwa sababu ya maji. Tumepata madhara makubwa sana kwa sababu ya maji, maana uchafu unakuja wa kila aina tunashindwa tufanyeje,  ila hatuna namna."

Pamoja na kukiri madhila ya ongezeko hilo Rose anaamini sababu kuu ya hali hii ni ongezeko la mvua tofauti na miaka iliyopita akisema ya kwamba, "ndio hivyo mwaka  huu Mungu ameleta mvua nyingi. Mimi naamini ni mvua hakuna kitu kingine kwa sababu hata kwenye redio unasikia wanatangaza mikoa mingine inanyesha kuanzia asubuhi mpaka jioni. Ni mvua tu ndio imekuwa nyingi mwaka huu."

Kwa upande wake Bernad Abel ambaye ni Msimamizi wa moja ya mialo anasema hali hii haikuwahi kushuhudiwa kwa hivi karibuni  akisema kuwa, "kwa mfano mwaka wa 2017 maji yaliingia lakini yaliingia mwezi wa Januari na Februari, kwa hivyo mwezi wa Juni, maji yalikuwa yameisha. Lakini kwa jinsi yalivyoingia hapa hatujui yatapungua lini kwa vile maji yalioingia ni mengi sana hayajawahi kutokea. Kwa hivyo hatujui yatapungua na kurudi lini pengine labda mwakani mvua tena ikanyesha . Mwaka huu hatujui kama yatapungua. Hii hali imeanza mwezi wa Novemba,  maji yameanza kuingia, kila siku maji tunaona yaongezeka."

Hata hivyo Bi. Rose anaamini serikali inaweza kufanya jambo kupunguza athari hizi, "serikali tunaomba tu, cha kwanza maji yasituathiri sana kama ni kukomea hapo, na serikali iangalie waathiriwa kama sisi mama lishe, kwa vile unaona wengine wamefikia kufunga vibanda vyao. Tunaomba tu labda mkubwa wetu atuangalie na kwamba hawa wapendwa wangu niwasaidieje."

 

Taarifa hii imeandaliwa na Ahimidiwe Olotu wa UNIC Dar es salaam