Afya ya akili ni msingi wa kila kitu kwenye COVID-19 - Guterres

14 Mei 2020

Ugonjwa wa virusi vya Corona ukiendelea kutikisa dunia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezindua muhtasari wa mkakati wa kushughulikia afya ya akili ambayo hivi sasa inatetereka kutokana na janga la COVID-19.
 

Katibu Mkuu amesema kuwa afya ya akili ni msingi wa ubinadamu na inawezesha kila mtu kufikia ustawi wake na kushiriki kwenye jamii. 
Hata hivyo amesema, COVID-19 siyo tu inadhoofisha afya ya mwili bali pia inaongeza machungu ya kifikra. Kupoteza wapendwa, mshtuko wa kupoteza ajira, kutengwa na zuio la kutembea, masahibu katika familia na sintofahamu ya mustakabali wa baadaye.”
Katibu Mkuu amesema matatizo ya afya ya akili, ikiwemo msongo wa mawazo na wasiwasi ni baadhi ya machungu makubwa ya ulimwengu wa sasa akisema kuwa baada ya miongo kadhaa ya kupuuzwa na uwekezaji hafifu kwenye huduma za afya ya akili, janga la COVID-19 sasa linagonga familia na jamii,  na walio hatarini zaidi ni wahudumu wa afya, wazee, barubaru, vijana na wale walio na shida za kiafya na walio kwenye mizozo.
Ni kwa kuzingatia hilo Katibu Mkuu amezindua muhtasari wa sera ya COVID-19 na afya ya akili akiongeza kuwa, “huduma za afya ya akili ni sehemu muhimu ya hatua za serikali za kukabili COVID-19. Lazima zipatiwe fedha za kutosha. Sera lazima zisaidie na kuhudumia walioathiriwa na mazingira ya kiafya na kulinda haki zao na utu. Kuzuiliwa ndani na karantini zisilenge kubagua wale walio na afya dhoofu ya akili.”
Katibu Mkuu amesema jamii inapoondokana na janga la Corona, ni lazima ielekeze sasa huduma za afya ya akili kama sehemu ya huduma ya afya kwa wote.
Amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake umeazimia kuweka dunia ambamo kwayo kila mtu, kila pahali ana mtu wa kumwelezea masahibu yake kuhusu afya ya akili.
 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud