Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Burundi yamfurusha Mkuu wa WHO siku chache kabla ya uchaguzi mkuu, WHO yazungumza

Dkt. Walter Kazadi Mulombo, Mwakilishi wa WHO nchini Burundi, ( wa pili kushoto) wakati wa uzinduzi wa wiki ya afya ya mama na mtoto mwaka 2019 nchini humo.
WHO/Burundi
Dkt. Walter Kazadi Mulombo, Mwakilishi wa WHO nchini Burundi, ( wa pili kushoto) wakati wa uzinduzi wa wiki ya afya ya mama na mtoto mwaka 2019 nchini humo.

Burundi yamfurusha Mkuu wa WHO siku chache kabla ya uchaguzi mkuu, WHO yazungumza

Masuala ya UM

Shirika la afya la Umoja la Umoja wa Mataifa, WHO, limesema linawasiliana na serikali ya Burundi ili kufahamu sababu ya kufukuzwa kwa mwakilishi wake nchini humo pamoja na wafanyakazi wengine watatu. Serikali ya Burundi ilitangaza jana kumfukuza mwakilishi huyo Dkt. Walter Kazadi Mulombo, ikiwa ni siku chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini humo. 

Hatua ya kufukuzwa kwa Dkt. Mulombo na wafanyakazi wengine watatu wa WHO imekuja siku chache baada ya shirika hilo kuelezea hofu yake ya kuhusu mikusanyiko ya kampeni za kisiasa nchini Burundi wakati huu wa  janga la virusi vya corona au COVID-19. Loise Wairimu na ripoti kamili.

Taarifa iliyotolewa leo na ofisi ya mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa katika eneo la maziwa Makuu imesema barua iliyoandikwa na wizara ya mambo ya nje ya Burundi imesema Mwakilishi wa WHO Burundi Dkt. Walter Kazadi Mulombo ni mtu asiyekubalika nchini humo, na ni lazima aondoke katika taifa hilo la Afrika Mashariki ifikapo Ijumaa wiki hii pamoja na wataalam wengine watatu wa WHO.

Hata hivyo barua hiyo haikutoa maelezo zaidi au sababu za kufurushwa kwao na Dkt. Mulombo hakupatikana kuweza kufafanua kuhusu tukio hilo.

Kufuatia taarifa hizo, Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amezungumza hii leo akisema kuwa amepokea taarifa za kuwepo kwa barua hiyo jana jumatano.
Amesema WHO inawasiliana na serikali ya Burundi ili ifafanue na iwaeleweshe sababu za uamuzi huo na wakati huo huo Umoja wa Mataifa nchini humo inapanga mipango ya kuondoka kwa mtendaji huyo.
Dkt. Moeti amekumbusha kuwa WHO iko tayari kuendelea kushirikiana na Burundi kama mwanachama wa WHO kanda ya Afrika katka siyo tu kukabiliana na COVID-19, bali pia katika mipango mingine ya afya.