Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katikati ya COVID-19, WFP yaendelea kunusuru wahitaji

Mke wa Bwana Sawadogo akiandaa chakula baada ya kupata mgao kutoka WFP huko Kaya, nchini Burkina Faso.
WFP/Mahamady Ouedraogo
Mke wa Bwana Sawadogo akiandaa chakula baada ya kupata mgao kutoka WFP huko Kaya, nchini Burkina Faso.

Katikati ya COVID-19, WFP yaendelea kunusuru wahitaji

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula, WFP, linaendelea kusaka rasilimali ili liweze kufikisha misaada kwa watu milioni 100 kwa mwaka huu 2020.

Misaada hiyo ikiwemo ya chakula ni muhimu kwa jamii zilizo hatarini ambapo WFP inasema kuwa kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii ni muhimu ili watu wengine milioni 130 wasitumbukie kwenye njaa kutokana na janga la virusi vya Corona au COVID-19.


Idadi hiyo ni kando ya watu wengine milioni 135 ambao tayari wamekuwa wanakabiliwa na njaa kabla ya janga la Corona.


WFP kwa kutambua umuhimu wa kuchukua hatua mapema, ilizindua vituo vyake vya kusheheni misaada ambacho kimojawpo kipo mjini Liège nchini Ubelgiji.


Shehena kutoka kituo hicho vikiwemo vifaa vya matibabu na vile ya kujikinga kama vile barakoa na glovu vimeshawasili Burkina Faso, vikiwa vimeratibiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na kamati ya msalaba mwekundu, ICRC.


Katika eneo la Kaya nchini Burkina Faso ambako watu waliokimbia makazi yao wamesaka hifadhi, UNICEF inaelimisha watu mbinu za kujikinga na Corona huku ikiwapatia msaada wa fedha za kujikimu.


Miongoni mwao ni Sawadogo Salam mwenye umri wa miaka 39 ambaye alikimbia makazi yake huko Arbinbda baada ya kundi la watu wenye silaha kushambulia kijiji chao na kuua wanakijiji kadhaa.


Alitembea kilometa 160 kwa mguu hadi Kaya ambapo familia yake ilifuata baadaye, lakini hadi leo hii watoto wake hawajaanza kwenda shuleni.


Sawadogo anasema kuwa, “tulikimbilia hapa kukwepa mauaji. Wanawake waliweza kuja baadaye na virago vichache. Tuliacha vitu vyote vikiwemo vyakula na vyombo vya jikoni.”


Angalau sasa fedha kutoka WFP zimemwezesha kununua chakula na mlo kwa familia unawezekana.


Margot Vandervelden ni Mkurugenzi wa WFP Idara ya masuala ya dharura na anasema kuwa,  dharura kama hizo zisizotaraijwa zinahitaji hatua za kimataifa na WFP inaongozza na kuchochea hatua za kimataifa kwa kuweka na kusambaza misaada ya kuokoa maisha kwa wanaohitaji. 


Hata hivo anasema, “lakini WFP inasafirisha kwa ndege vifaa vya matibabu na wahudumu wa misaada kutoka jamii yote ya usaidizi wa kibinadamu na afya. Lakini ni dhahiri tunahitaji fedha ili tuweze kufanya hivyo.”