Ni wakati wa dini zote kushirikiana katika kupambana na COVID-19 

12 Mei 2020

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo kwa njia ya video amekutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wakuu wa kidini duniani katika mkutano wa ngazi ya juu kuhusu jukumu la viongozi wa kidini katika kushughulikia changamoto za ugonjwa wa COVID-19. 

Bwana Guterres amesema, "wakati virusi vinaleta zahma kwa kiwango ambacho hakijawahi kuonekana kwa vizazi kadhaa, tunaona tofauti ambazo mara nyingi hutugawanya ni za maana. Na inaonyesha utu wetu wa pamoja. "

Katika hotuba yake Guterres amesema ugonjwa huo "haujali tofauti za kidini au za kiroho. Haujali mipaka ya kitaifa. Sisi sote ni wanyonge - na kwamba mazingira hayo hatarishi yanaonyesha ubinadamu wetu wa kawaida."

Katibu Mkuu Guteress ameongeza kuwa virusi vinaweka jukumu letu la kukuza mshikamano kama msingi wa majibu yetu - mshikamano unaotegemea haki za binadamu na utu wa binadamu. Aidha amewataka  viongozi wa kidini kupinga ujumbe ambao unakuwa siyo sahihi na wenye kuumiza na pia wakatae ubaguzi, ubaguzi wa rangi na kila namna ya kutokuvumiliana. 

Bwana Guterres amesisitiza maeneo manne ambayo viongozi wa kidini wana mchango mkubwa katika kutoa suluhisho kwa si tu kushughulikia janga lakini katika kurejea katika hali yetu vizuri. Hii inajumuisha kuunga mkono ombi lake la kusitisha mapigano kimataifa na ombi lake la amani majumbani kuhusiana na kuongezeka manyanyaso dhidi ya wanawake na wasichana wakati janga la virusi vya corona na kujifungia kunavyoongezeka. 

Kwa upande wa viongozi wa kidini, Kaldinali Miguel Ángel Ayuso Guixot, ambaye ni Rais wa Baraza la Maaskofu wa Vatican kwa ajili ya mazungumzo ya dini mbalimbali amesema huu hauwezi kuwa wakati wa ubinafsi na kugawanyika, akiongeza kuwa watu wamekuwa wamoja zaidi na wameelewa kuwa maisha maisha ya jamii tofauti yanategemeana kama sehemu ya familia ya binadamu “tunategemeana. Mtazamo wetu wa kuhisi umoja sio kutoka kwa nguvu ya kiuchumi au ya mikono, haswa ni kwa kuwa tumejigundua tu wadhaifu na kwa hivyo tunahitajiana.”

Naye Kiongozi Mkuu  wa Sinagogi la mjini New York Marekani Arthur Schneier amesema, imani, sala, na hatua zinaweza kujenga mustakabali mzuri, akiongeza kuwa historia ya pamoja ya ubinadamu inaonyesha kwamba binadamu huibuka kila wakati.

“Kama viongozi wa dini, hatuwezi kutatua changamoto za matibabu na machafuko ya kiuchumi yanayosababishwa na janga hili. Tunaweza na lazima tuongeze juhudi zetu za kuunganisha familia iliyogawanyika, na kuwakumbusha watu wetu – wakati huu zaidi ya hapo zamani - mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe na umheshimu mwingine." Amesema Schneier. 

Kwa upande wake Profesa Ahmed Abbadi, Katibu Mkuu wa Rabita Mohammadia ya Maulama wa Ufalme wa Moroko, amesema viongozi wa dini na taasisi wana jukumu kubwa katika kukuza ufahamu, mshikamano, utulivu, hekima, umoja, mwongozo, udugu, miongoni mwa matendo mengine mema na maadili. Amesema hii ndio, "chanzo cha kuaminika kwa viongozi wa dini na taasisi, lakini tunahitaji kukumbuka kuwa hali kubwa ya lazima na ya wazi ilionekana katika hali hii iliyosababishwa na COVID-19, ambalo ni hitaji la dijitali."

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter