Ghasia Nigeria zasababisha  raia 23,000 wakimbilie Niger mwezi Aprili pekee- UNHCR

12 Mei 2020

Ghasia zinazoendelea kaskazini-magharibi mwa Nigeria zimelazimisha watu wapatao 23,000 kukimbia nchi yao na kusaka hifadhi nchi jirani ya Niger kwa mwezi uliopita wa Aprili pekee. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linasema kuwa idadi hii inafanya raia wa Nigeria waliokimbilia Niger tangu mwezi Aprili mwaka jana iwe zaidi ya 60,000. 
 

Msemaji wa UNHCR Babar Baloch akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya video, amesema kuwa watu hao waliosaka hifadhi katika eneo la Maradi nchini Niger, wanakimbia mashambulizi kutoka vikundi vilivyojihami kwenye majimbo ya Sokoto, Zamfara na Katsina nchini Nigeria, na kuongeza shinikizo kwa wakimbizi wa ndani elfu 19 wa Niger, waliosalia wakimbizi ndani ya nchi yao.
 
Bwana Baloch anasema kuwa, UNHCR inahofia kuendelea kudorora kwa usalama nchini Nigeria na uwezekano wa mashambulizi hayo kusamaa hadi Niger.
 
Kwa mujibu wa UNHCR idadi kubwa ya wakimbizi wa sasa kutoka Nigeria ni wanawake na watoto ambao wanakimbia mashambulizi, wakisema kuwa, kuna ukatili wa kupita kiasi ikiwemo mauaji ya raia, kutekwa nyara ili jamaa walipe fedha, uchomaji moto nyumba na uporaji wa mali.
 
Licha ya mpaka kufungwa kutokana na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19, wakimbizi kutoka Nigeria, wameruhusiwa kusaka hifadhi Niger na sasa mahitaji yao ni maji, chakula na huduma za afya pamoja na makazi na malazi.
 
Wakimbizi hao waliojikuta kwenye mapigano, wanalaumu wakulima na wafugaji kutoka makabila mbalimbali.
 
Bwana Baloch amesema wanachofanya sasa wao ni kushirikiana na mamlaka nchini Niger ili kuhakikisha wakimbizi wapatao 7,000 wanahamishiwa maeneo salama ambako ni kwenye vijiji vilivyopo kilometa 20 kutoka mpakani ili wapatiwe huduma za msingi.
 
 

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter