Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hofu ya COVID-19 yaambatana na hofu ya ukatili majumbani huko Cox’s Bazar

Wakimbizi warohingya bado wanaishi wilaya ya Cox's Bazar nchini Bangladesh miaka kadhaa tangu wakimbie nchi yao ya Mynamar
© UNFPA Bangladesh/Carly Learson
Wakimbizi warohingya bado wanaishi wilaya ya Cox's Bazar nchini Bangladesh miaka kadhaa tangu wakimbie nchi yao ya Mynamar

Hofu ya COVID-19 yaambatana na hofu ya ukatili majumbani huko Cox’s Bazar

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema ingawa ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19, unakwamisha harakati za kufuatialia visa vya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto katika kambi ya wakimbizi warohingya huko Bangladesh, bado kuna mbinu zinatumika kupatia msaada manusura.

Katika kambi ya wakimbizi wa kabila la warohingya kutoka Myanmar, iliyoko Cox’s Bazar nchini Bangladesh, hofu ya Covid-19 inaenda sambamba na ile ya ukatili wa majumbani.


Richa Biswas ambaye ni afisa wa ulinzi wa mtoto, UNICEF katika kambi hii anasema kutokana na janga la COVID-19, harakati za wafanyakazi wa huduma za kibinadamu za kutembelea kambi kusaidia manusura wa ukatili zimepunguzwa kutokana na vizuizi vya kuepuka kuenea kwa Corona, na hii inatia hofu kwa wakimbizi akisema, “na kwa wanawake na wasichana, hali ni vivyo hivyo, wamefungiwa ndani na ukatili kutoka kwa  na wapenzi wao au ukatili wa majumbani unaweza kuongezeka pia majumbani.”


UNICEF inasema kuwa kambini, ukatili wa kijinsia unafanyika ndani ya nyumba ya manusura ambapo idadi kubwa ya visa vilivyoripotiwa ni kutoka kwa wanawake.
Bi. Biswas ameongeza kuwa kutokana na vizuizi, “kile ambacho tunaweza kufanya sasa ni kushughulikia kisa cha mtu mmoja mmoja, hii ikiwemo kuripoti ukatili na manyanyaso na pia kuelekeza mahali pa kupata huduma zaidi na msaada wa kisaikolojia.”


UNICEF inasema kuwa hofu ya wanawake na wasichana ni kwamba ulinzi na huduma utakoma lakini kinachofanyika ni kwamba imeweka mfumo wa mtandao kwa manusura kutoa ripoti ili kuhakikisha hakuna janga la kimyakimya katikati ya janga la kimataifa la COVID-19.