Tusipokuwa makini, COVID-19 itatowesha mafanikio dhidi ya UKIMWI-UN

11 Mei 2020

Janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19 linaweza kurejesha nyuma mafanikio yaliyopatikana katika kutokomeza ugonjwa wa virusi vya Ukimwi, AIDS, yamesema mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la afya, WHO na lile la kukabiliana na UKIMWI, UNAIDS.

Taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi na kuchapishwa katika wavuti wa UNAIDS inasema kuwa kundi lililoundwa kufanya makadirio ya athari hizo limesema kuwa, “iwapo hatua hazitachukuliwa za kutosha kupunguza na kukabili mvurugano wa huduma za afya na vifaa vya tiba wakati wa janga la COVID-19, hali hiyo ya ukosefu wa dawa za kupunguza makali ya VVU ikidumu kwa miezi 6, basi kunaweza kukawepo na nyongeza ya vifo zaidi ya 500,000 kutokana na magonjwa yahusianayo na Ukimwi ikiwemo Kifua Kikuu kwa mwaka 2020/2021 katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.”

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema kuwa makadirio hayo machungu ya wamba watu nusu milioni katika nchi za Afrika watakufa kwa Ukimwi, ni sawa na kurejea katika historia akiongeza kuwa, “lazima tuone hili kama kengele ya kutuamsha ili tubaini mbinu za kusongesha huduma muhimu za afya. Kwa Virusi Vya Ukimwi, VVU, baadhi ya nchi tayari zinachukua hatua muhimu, mathalani, kuhakikisha watu wanaweza kupata kiasi kikubwa cha dawa zao na vifaa vingine kama vile vya kujipima,ili kuondoa shinikizo kwa huduma za afya na wahudumu wa afya. Tunapaswa kuhakikisha kuwa vifaa na tiba vinapatikana katika nchi ambazo zinahitaji zaidi.”

Katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, takribani watu milioni 25.7 walikuwa wanaishi na VVU na wengine milioni 16.4, sawa na asilimia 64 walikuwa wanapatiwa dawa za kupunguza makali ya VVU mwaka 2018.

Hata hivyo, UNAIDS na WHO wanasema kuwa watu hao hivi sasa wako hatarini kwa kuwa huduma dhidi ya VVU zimefungwa au zimeathirika kwa sababu huduma nyingi zimeelekezwa kwenye vita dhidi ya COVID-19.

Mashirika hayo yanasema kuwa mafanikio yaliyopatikana katika kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto, yanaweza kurudishwa nyuma ambapo maambukizi hayo miongoni mwa watoto yanaweza kuongezeka kwa takribani asilimia 104.

Ni kwa mantiki hiyo, Winnie Byanyima, Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS anasema kuwa, “COVID-19, isiwe kisingizio cha kuengua uwekezaji kutoka VVU. Kuna hatari kubwa kwamba mafanikio yaliyopatikana kwa taabu katika kuondokana na Ukimwi, yanaweza kuwekwa rehani kwa sababu ya vita dhidi ya janga la Corona, lakini haki ya huduma ya afya inaamaanisha kuwa hakuna ugonjwa ambao unapaswa kupigwa vita kuliko mwingine.”

UNAIDS inakumbusha kuwa pindi tiba kwa mtu anayeishi VVU inapofuatwa ipasavyo, hufika wakati virusi vinakuwa haviwezi kuonekana na hivyo kuzuia kuendeleza maambukizi vya virusi hivyo, na kwamba mvurugiko kidogo wa matibabu unaweza kuwa na madhara makubwa kwa afya ya mgonjwa na hivyo kuweza kuambukiza VVU.

Utafiti ulihusisha majopo matatu ya wabobezi wakitumia mbinu mbalimbali kuchambua madhara ya kuvurugwa kwa huduma za uchunguzi, tiba na kinga dhidi ya VVU kunakosababishwa na uwepo wa janga la COVID-19.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud