Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfanyakazi yuko njia panda : Afe kwa njaa au virusi? - ILO

Mfanyikazi akifanyakazi katika Kampuni ya Clean World akitoa mabaki ya sabuni inayotoka katika ukanda wa conveyor
ILO Photo/John Isaac
Mfanyikazi akifanyakazi katika Kampuni ya Clean World akitoa mabaki ya sabuni inayotoka katika ukanda wa conveyor

Mfanyakazi yuko njia panda : Afe kwa njaa au virusi? - ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Mikakati ya kutaka watu kubaki majumbani ili kuzuia kuenea kwa virusi vya ugonjwa wa Corona au COVID-19 imewaweka wafanyakazi njia panda akiwa hafahamu achague afe njaa na familia yake au afe kwa virusi.

Mikakati ya kutaka watu kubaki majumbani ili kuzuia kuenea kwa virusi vya ugonjwa wa Corona au COVID-19 inatishia kuongeza kwa asilimia 56 viwango vya umaskini miongoni mwa wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi walioko nchi za kipato cha chini.

Shirika la kazi  la Umoja wa Mataifa, ILO limesema hayo katika nyaraka yake mpya wakati huu ambapo mataifa kadhaa yamechukua hatua kali kuzuia watu kutoka majumbani ikiwemo hata kufanya biashara ndogo ndogo kama njia ya kudhibiti COVID-19.

ILO inaesema kiwango hicho cha ongezeko la umaskini kwa asilimia 56 kati nchi hizo za kipato cha chini ni kikubwa ukilinganisha na asilimia 52 nchi za kipato cha juu na asilimia 21 kwa walioko nchi za kipato cha kati.

Shirika hilo linasema kuwa, “takribani wafanyakazi bilioni 1.6 wa sekta isiyo rasmi kati ya wafanyakazi bilioni 2 wa sekta hiyo duniani kote, wameathiriwa na hatua za kukaa ndani au kutotembea hovyo. Wengi wao wako kwenye sekta zilizoathiriwa zaidi au kwenye maeneo ambayo kuna madhara makubwa. Sekta hizo ni pamojana zile za malazi, chakula, uzalishaji, biashara ya jumla na rejareja na zaidi ya wakulima milioni 500 wanaozalisha chakula kwa ajili ya wakazi wa mijini.”

Ripoti inasema kuwa wanawake ndio wamekumbwa zaidi kwenye sekta hizo na kwamba, “wakati wafanyakazi wakihitaji kufanya kazi kulisha familia zao, hatua za kudhibiti COVID-19 katka nchi nyingi haziwezi kutekelezwa ipasavyo. Hii inaathiri juhudi za serikali za kulinda jamii na kukabiliana na janga.”

Kama hiyo haitoshi, ILO inasema mvutano huo unaweza kuleta mvurugano katiika nchi ambako sekta isiyo rasmi ni kubwa.

“Wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi wakiwa hawana mbinu yoyote ya kusaidia familia zao, wanabakia kwenye mkanganyiko, wafe kwa njaa au kwa virusi,”  imesema ripoti hiyo ikiongeza kuwa hali inakuwa mbaya kutokana na kuongezeka kwa uhaba wa chakula ambao unakumba zaidi wale waliokuwa kwenye sekta isiyo rasmi.

Ikimulika wafanyakaiz wa ndani, ripoti inasema kuwa kwa wafanyakazi hao milioni 67 ambao asilimia 75 kati yao wako kwenye sekta isiyo rasmi, suala la ukosefu wa ajira limekuwa tishio kama vilivyo virusi vyenyewe vya Corona.

“Wengi wao hajawaweza kufanya kazi, iwe kwa ombi la waajiri wao au kwa zuio la kudhibiti kuenea kwa Corona. Wale ambao wanaendelea na ajira, wako hatarini zaidi kuambukizwa Corona wakihudumia familia kwenye makazi binafsi. Kwa wafanyakazi wa ndani wahamiaji milioni 11 hali ni mbaya zaidi,”  imesema ripoti hiyo.

Akizungumzia ripoti hiyo, Philippe Marcadent, Mkuu wa kitengo cha sekta isiyo rasmi, ILO amesema kuwa, “Janga la COVID-19, linaongeza ukosefu wa usawa ambao tayari ulikuwepo. Hatua za kisera lazima zihakikishe msaada unafikia wafanyakazi na kampuni zenye uhitaji zaidi.”

Kimaeneo, hatua za kuzuia watu kutochangaman zimekuwa na madhara zaidi huko Amerika ya Kusini ikifuatiwa na nchi za kiarabu, halafu Afrika, kisha Asia na Pasifiki na Ulaya na Asia ya Kati.

ILO inapendekeza kuwa nchi zinapaswa kufuata mkakati mchanganyiko unaozingatia athari zote za kiafya na kiuchumi.

Kwa mantiki hiyo, nchi zinatakiwa kuwa na sera zinazopunguza fursa za wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi kupata maambukizi ya virusi, kuhakikisha wale wanaoambukizwa wanapata huduma ya afya, kuwapatia msaada wa kipato na chakula wao na familia zao pamoja na kuzuia hali ya sasa isilete madhara ya kudumu ya kiuchumi.