Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machifu Niger wapita mtaa kwa mtaa kuelimisha watu kuhusu COVID-19

Yayé Modi akiwa amemtembelea mmoja wa wakazi wa kitongoji cha mji mkuu wa Niger, Niamey akimuelimisha kuhusu virusi vya Corona.
© UNICEF/UNI322710/Haro
Yayé Modi akiwa amemtembelea mmoja wa wakazi wa kitongoji cha mji mkuu wa Niger, Niamey akimuelimisha kuhusu virusi vya Corona.

Machifu Niger wapita mtaa kwa mtaa kuelimisha watu kuhusu COVID-19

Afya

 Nchini Niger, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linashirikiana na viongozi wa kijadi kusaidia kuelimisha jamii ijikinge dhidi ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19, katika taifa hilo ambako tayari kuna wagonjwa 763 na kati yao hao, 38 wamefariki dunia. Maelezo zaidi na Loise Wairimu.

Hatua hiyo ya UNICEF inazingatia kuwa taifa hilo la Afrika hadi sasa lina wagonjwa waliothibitishwa 763 wa Corona, na kati yao, 38  wamefariki dunia.

Kampeni zinafanyika katika vitongoji vya mji mkuu wa Niger, Niamey ambapo viongozi wa kijadi na wapiga debe wanaelimisha umma, kufuatia msaada kutoka UNICEF.

Mfanyakazi wa UNICEF akisaidia kampeni ya kuhamasisha umma kuhusu COVID-19
© UNICEF/UNI322709/Haro
Mfanyakazi wa UNICEF akisaidia kampeni ya kuhamasisha umma kuhusu COVID-19

 

Miongoni mwa viongozi hao wa jadi ni Yaye Modi Alzouma, Chifu wa eneo la Banizoumbou mjini Niamey,  ambaye anasema kuwa, “tangu kuingia kwa huu ugonjwa huu wa Corona, tumekuwa tukifanya kazi kuongeza uelewa. Tunatuma magari yenye vipaza sauti kwenye makazi ya watu. Niamey ni mji mkubwa, kwa hiyo hatuwezi kutembea mguu kwa mguu. Ni kwa kutumia magari yenye vifaa mahsusi tunaweza kuelimisha watu. Watu wanasikiliza machifu. Machifu ndio wanawaelezea jinsi ya kuchukua hatua. Watu bado wanajaribu kuelewa hali ilivyo. Wakati wa sherehe za ubatizo au harusi, hawakusanyiki kwa sababu ya huu ugonjwa.”

Lengo la mpango huu ni kuhamasisha jamii ili ielewa na izingatie kanuni za kutochangamana, na kuheshimu amri ya dharura ya kutotembea hovyo.

 

Harouna Bague ambaye ni mpiga debe anasema kuwa matumizi ya magari yenye vipaza sauti ni muhimu kwa sababu, “watu wengi hawana televisheni wala radio na si kila mtu anaweza kufuatilia taarifa kupitia vyombo hivyo vya habari. Iwapo watu 5 watatusikiliza, wataweza kusambaza ujumbe huo kwa watu wengine 100 na kadhalika.”