Ukata na COVID-19 vyatishia huduma za afya ya uzazi  Yemen- UNFPA

6 Mei 2020

Fikiria kuwa kila baada ya saa 2, mwanamke mmoja anafariki dunia nchini Yemen akiwa anajifungua. Kama hiyo haitoshi, wale wanaobahatika kujifungua salama, 20 kati yao watakumbwa na majeraha, maambukizi, ulemavu, mambo ambayo yanaweza kuepukika.

Hiyo ni kauli ya Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu, UNFPA, Natalia Kanem, aliyoitoa kupitia taarifa iliyochapishwa leo jijini New York, Marekani.
Dkt. Kanem anasema kuwa, hali hiyo halisi inatokana na ukweli kwamba mfumo wa afya Yemen umesambaratishwa na mapigano yanayoendelea na zaidi ya yote janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19 linatumbukiza wajawazito na watoto wanaozaliwa kwenye shida kubwa zaidi.

“Zaidi ya wanawake 48,000 nchini Yemen watakufa kutokana na shida zitokanazo na ujauzito au kujifungua nchini Yemen, ambako kuna janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani, kutokana na ukata na uwezekano wa kufunga baadhi ya vituo vya afya kutokana na hofu ya maambukizi ya Corona,” amesema Dkt. Kanem.

Mkunga akihudumia wagonjwa
UNFPA Yemen
Mkunga akihudumia wagonjwa

UNFPA inasema inataka kuokoa maisha na hivyo inaomba dola milioni 59, zitakazotumiwa hadi mwishoni mwa mwaka huu wa 2020 “ili kutoa huduma za afya za kuokoa maisha ya . Nyongeza ya dola milioni 24 inahitajika pia ili kulinda wafanyakazi wa afya dhidi ya virusi vya Coronana pia kuwezesha wanawake na wasichana kupata huduma za afyaya uzazi.”

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa UNFPA anasema kuwa iwapo huduma za afya ya uzazi zikisitishwa nchini Yemen,  hali itakuwa mbaya kwa wanawake na wasichana.

Mfumo wa afya Yemen umesambaratika

Hivi sasa nchini Yemen, takribani nusu ya vituo vya afya havifanyi kazi kabisa au vinatoa huduma kidogo. Ni asilimia 20 tu ya vituo vya afya vinatoa huduma za afya ya mama na mtoto kutokana na uhaba wa wafanyakazi, vifaa vya matibabu, na ukosefu wa fedha ambapo wahudumu wa afya hawajalipwa mishahara yao au wamelipwa kidogo tu kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.

Tukikosa fedha tunafunga vituo- UNFPA

UNFPA inasema kuwa ukata utalazimu wasitishe huduma za afya ya uzazi katika vituo 140 vya afya nchini Yemen. “Iwapo huduma hizo zitakoma, takribani wajawazito 320,000 watashindwa kupata huduma za uzazi na zaidi ya 48,000 wanaweza kufariki dunia wakati wa kujifungua.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter