Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaonya kuhusu ukatili na unyanyasaji wa Watoto wakati huu wa COVID-19

Mahery mvulana wa miaka nane alinyanyaswa mara kwa mara na mama yake huko Mahajanga, Madagaska.
© UNICEF/Abela Ralaivita
Mahery mvulana wa miaka nane alinyanyaswa mara kwa mara na mama yake huko Mahajanga, Madagaska.

UN yaonya kuhusu ukatili na unyanyasaji wa Watoto wakati huu wa COVID-19

Haki za binadamu

Umoja wa Mataifa umesema kuna haja ya haraka ya huduma ya kuwalinda watoto ili kupunguza hatari ya ukatli wa kingono na unyanyasaji mwingine kote duniani hasa wakati huu mamilioni wakisalia nyumbani kutokana na janga la virisi vya corona au COVID-19

Katika taarifa iliyotolewa leo mtaalam maalum wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uuzaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto Mama Fatima Singhateh, ameonya kwamba ripoti za ongezeko la machafuko dhidi ya watoto na mifumo mingine ya unyanyasaji wa kingono na ukatili wakati huu wakisalia majumbani sababu ya COVID-19, vitakuwa na athari za muda mrefu kwa mamilioni ya watoto hao kote duniani.

Ameongeza kuwa“kati ya watoto milioni 42 na milioni 66 kote dunini tayari wako katika hali mbaya ya kiuchumi na kijamii hata kabla ya athari zilizojificha za janga jipya la COVIDI-19. Hivyo athari za janga hili kwa mamilioni ya watoto zitakuwa mbaya sana endapo tutakuwa wazito kuchukua hatua za huduma za kuwalinda kwa ajili ya kuubaini mapema na kuuzuia ukatili huo.”

Mama Singhaten amesisitiza kuwa ni muhimu sana kuwa na picha kamili na hatua za ulinzi wa haraka kwa watoto, ili kutathimini ukubwa wa tatizo hili hususan kwa watoto walio katika mazingira hatarishi ikiwa ni pamoja na wakimbizi, wakimbizi wa ndani, wasio na makazi, wahamiaji, walio katika makundi ya wachache, wanaoishi katika makazi duni, watoto wa mitaani, wanaoishi katika makazi ya wakimbizi na wale wanaoishi katika vituo vya kulelea watoto.

Mtaalam huyo amesema vikwazo vya kusafiri kwa sababu ya COVID-19 vimeibua mifumo mipya ya unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto ikiwemo majaribio ya huduma za kuwasafirisha au kuwapeleka watoto kwa magari kwa ajili ya kufanyiwa ukatili wa kingono.

Ameongeza kuwa “Pia kumekuwa na ongezeko la idadi ya majaribio ya kuingia katika wavuti zilizo na picha ua video za watoto wakifanyiwa ukatili wa kingono. Kutengeneza picha hizo au kuzionyesha moja kwa moja mtandaoni sasa imekuwa njia rahisi na mbadala ya kuwaingiza watoto katika mtandao na shughuli za kingono na kuuza picha zao katika jamii ya mtandaoni.”

Hivyo amesema hatua zisipochukuliwa sasa basi janga la COVID-19 litawaacha ambao tayari wako nyuma kubaki nyuma zaidi na kukiuka ahadi iliyowekwa na malego ya maendeleo endelevu SDGs ya kutomuacha yeyote nyuma, ahadi ambayo sasa ni muhimu kuliko wakati mwingine wowote.