Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wauguzi na wakunga huduma ya usafi iko mikononi mwenu:WHO

Mkunga Msaidizi aosha mikono yake kabla ya kumhudumia mwanamke mjamzito kama ilivyo ada ya Siku ya Afya ya Kijiji na Lishe huko Shrawasti, India.
UNICEF/Vishwanathan
Mkunga Msaidizi aosha mikono yake kabla ya kumhudumia mwanamke mjamzito kama ilivyo ada ya Siku ya Afya ya Kijiji na Lishe huko Shrawasti, India.

Wauguzi na wakunga huduma ya usafi iko mikononi mwenu:WHO

Afya

Katika kuadhimisha siku ya usafi wa mikono hii leo shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO linawachagiza watu kote duniani kuongeza juhudi za kuhakikisha usafi wa mikono katika vituo vya afya ili kuwalinda wahudumu wa afya na wagonjwa dhidi ya maambukizi. 

Shirika la WHO linasema maadhimisho ya mwaka huu yanajikita na kaulimbiu “Okoa maisha:wauguzi na wakunga huduma ya usafi iko mikononi mwenu” ikienda sanjari na mwaka wa wauguzi na wakunga na lengo kuu ni kutambua mchango wa wahudumu hao wa afya kama mashujaa walio msitari wa mbele, kuwashukuru na kutanabaisha jukumu kubwa walilonalo katika kuzuia maambukizi .

Elizabeth Iro ni mkuu wa wauguzi katika shirika la WHO anaeleza sababu ya kuihusisha siku ya mwaka huu na wauguzi na wakunga.

“Sio tu kwamba tunataka kuchagiza usafi wa mikono , kuzuia maambukizi na hulka ya kuyadhibiti lakini pia tunataka kutambua jukumu muhimu walilonalo wauguzi na wakunga katika kuzuia maambukizi yanayoweza kuepukika”

Ameongeza kuwa wauguzi na wakunga ni muhimu sana kwani

“Kama kundi kubwa kabisa la wahudumu wa afya wanaotoa huduma kwa wagonjwa, wauguzi na wakunga ni muhimu katika kutoa huduma ya usafi. Katika nchi nyingi wanaoongoza katika kudhibiti maambukizi ni wauguzi hivyo wana nafasi kubwa katika kuzuia maambukizi hayo”

Na kuhusu kuzingatia usafi wa mikono Elizabeth anasema

“Usafi wa mikono ni hatua moja muhimu na inayofanyakazi unayoweza kuichukua kupunguza kusambaa kwa vijidudu na kuzuia maambukizi, ikiwemo virusi vya COVID-19”

Siku ya usafi wa mikono ilianza kuadhimishwa rasmi mwaka 2009 na tangu hapo hufanyika kila mwaka tarehe 5 Mei.