COVID-19 imetugeuza wafungwa, sina mtandao wa kufuatilia masomo - Mtoto DRC

30 Aprili 2020

 Watoto nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, hivi sasa licha ya kutokwenda shuleni kutokana na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19, wanatumia muda huo kusoma nyumbani, kusaidia kazi sambamba na kuelimisha jamii ili ijikinge na virusi hivyo.

Kutana na mtoto Cornell Mbonyi, mkazi wa Goma jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Hapa amempigia simu mwenzake kumsalimu na kutaka kufahamu iwapo ana taarifa zozote za lini shule itafunguliwa kwani hata yeye Cornell hafahamu chochote.

Cornell mwenye umri wa miaka 12 anaishi na wazazi na nduguze wakati huu ambapo shule zimefungwa kutokana na janga la Corona.

Kupitia video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Cornell anaonekana akisaidia kazi mbalimbali ikiwemo kupanda mazao, kuuza genge la mbogamboga na viungo na pia kuchora na kwa bahati mbaya kama ilivyo kwa mamilioni ya watoto duniani, Cornell hana mtandao wa intaneti nyumbani..

“kwa hiyo mimi nasoma kwa kutumia vitabu vyangu vya shuleni, nafanya marejeo ya masomo na pia nasoma vitabu vya riwaya ambavyo nilitoka navyo shuleni. Janga hili la Corona limetuletea hali mbaya. Linasababisha tushindwe kwenda shule, kanisani na kufanya mambo mengine muhimu. Wakati mwingine najiona kama mfungwa.”

Huku muda wa kufungua shule ukiwa bado hautambuliki, Cornell anasema kuwa,

“Sifahamu ni lini tutaanza tena kwenda shuleni. Kwa hiyo naendelea kuwa makini na kumweleza kila mtu, nawa mikono yako kwa maji tiririka na sabuni na zingatia umbali pindi watu wanapozungumza.”

Tangu COVID-19 itangazwe kuwa janga duniani,takwimu inaonyesha kuwa hadi leo hii, DRC ina jumla ya wagonjwa 497 huku watu 30 kati yao hao wakifariki dunia.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud