Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka kutumikishwa vitani Sudan Kusini hadi kumiliki karakana ya samani

Malis, (si jina lake halisi) akiwa kwenye karakana yake kwenye eneo la Yambio jimboni Equatoria Magharibi nchini Sudan Kusini.
UNMISS\Denis
Malis, (si jina lake halisi) akiwa kwenye karakana yake kwenye eneo la Yambio jimboni Equatoria Magharibi nchini Sudan Kusini.

Kutoka kutumikishwa vitani Sudan Kusini hadi kumiliki karakana ya samani

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Sudan Kusini, watoto waliokuwa wametumikishwa vitani na hatimaye kuachiliwa huru sasa wameanza kubadili maisha yao na ya wengine baada ya kupatiwa stadi za kujipatia kipato kwa msaada wa Umoja wa Mataifa na wadau wake.

Nchini Sudan Kusini, watoto waliokuwa wametumikishwa vitani na hatimaye kuachiliwa huru sasa wameanza kubadili maisha yao na ya wengine baada ya kupatiwa stadi za kujipatia kipato kwa msaada wa Umoja wa Mataifa na wadau wake.

Miongoni mwa watoto hao ni Malis, si jina lake halisi ambaye sasa anamiliki karakana ya kutengenza samani huko Yambio  jimboni Equatoria Magharibi.

Malis ambaye sasa ana umri wa miaka 26 alitekwa nyara na kundi la watu wenye silaha akiwa bado barubaru  na kupelekwa msituni ambapo anasema kuwa, “wakati tulipokuwa msituni, tulipata shida sana. Amani ilipopatikana nchini mwetu, tulitoka msituni na kujisalimisha na pia tulipatiwa mafunzo.”

Mapema mwaka 2018, Malis alibahatika kwani aliachiliwa huru na watesi wake kufuatia harakati zilizoongozwa na vikundi vya kidini na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS.

Askofu Hiiboro Kusala wa kanisa katoliki Dayosisi ya Tombura na Yambio yeye ni mwenyekiti wa kikundi cha kidini na anazungumzia harakati za kuachiliwa kwa Malis na wenzake akisema kuwa, “tuliweza kukutana na watu hao msituni na kisha kuweza kuwatoa msituni zaidi ya vijana 10,000 ambao walikuwa wanashikiliwa huko, vijana ambao walikuwa tayari kuua na hata kupigana. Na ni kwamba mara nyingi, jambo ambalo sipendi kusema, vijana hao walikuwa wanatufanya manyanyaso sana msituni lakini hatukukata tamaa.”

Kunasuliwa msituni, kumewezesha hii leo Malis awe na stadi za ufundi seremala akiwa na cheti baada ya kumaliza mafunzo ya miezi 6 ya ufundi stadi yaliyofadhiliwa na UNMISS na wadau na kutekelezwa na shirika la World Vision katika chuo cha mafunzo stadi cha Tiindoka.

Malis anasema kuwa, “nilianza kujifunza jinsi wanavyopima vitu vyote mfano kukata na kuweka matundu. Nilijifunza vitu vyote hapo sasa naweza kutengeneza meza, viti na hata vitanda. Mtu anaweza kufika akapenda na tunazungumza na ananipatia fedha.”

Mafunzo yalimweza kuanzisha karakana yake na kutengeneza samani zinazohitajika kwenye jamii yake.

Malis si mchoyo wa ujuzi wake na hivyo katika karakana yake anafundisha vijana wengine, miongoni mwao ni Isaac ambaye naye si jina lake halisi na anasema kuwa, “amenifundisha mambo mengi. Hivi sasa naweza kutengeneza vitu vingi kama vile vitanda, milango, kabati na vitu vingine vingi vidogo vidogo.”

UNMISS kwa upande wake inajivunia kwa kuwa kwa kufanya kazi na wananchi wa Sudan Kusini katika kujenga amani ya kudumu ndio jukumu lake.

Christopher Muchiri Murenga, ni mkuu wa ofisi ya UNMISS mjini Yambio na anasema kuwa, “tunataka kujenga mashauriano kati ya jamii kuhusu kile walicho nacho na fursa za maendeleo kwenye jamii zao na changamoto wanazokabiliana nazo. Halikadhalika vitisho wanavyodhani wanawea kukumbana navyo na uthabiti na udhaifu wao ili hatimaye wao wenyewe wawe vichocheo vya kujenga mnepo na kusonga mbele katika kujikwamua na kuendelea.”

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, zaidi ya watoto 3,000 nchini Sudan Kusini wameachiliwa huru na vikundi vilivyojihami tangu kuanza kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini mwezi Disemba mwaka 2013 na bado maelfu kadhaa wanatumikishwa vitani.