Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je ni vipi biashara mtandaoni itakwamua nchi baada ya COVID-19?

Biashara mtandaoni inasaidia bidhaa kama hizi zinazotengenezwa huko huko Manzini, Swaziland kuweza kupatikana hata kwa wahitaji barani Asia
FAO/Giulio Napolitano
Biashara mtandaoni inasaidia bidhaa kama hizi zinazotengenezwa huko huko Manzini, Swaziland kuweza kupatikana hata kwa wahitaji barani Asia

Je ni vipi biashara mtandaoni itakwamua nchi baada ya COVID-19?

Ukuaji wa Kiuchumi

Wiki ya biashara mtandao ya kamati ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD ikianza hii leo, miongoni mwa mambo yanayoangaziwa ni jinsi ya kupata suluhu za kidijitali katika kusaidia dunia kujikwamua baada ya janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Ripoti mpya ya uchambuzi wa biashara mtandaoni iliyochapishwa katika wavuti wa UNCTAD inasema kuwa hatua hiyo inazingatia ukweli kwamba biashara ya mtandao inakua lakini bila uwiano katika mataifa yote.

Mathalani UNCTAD inasema kuwa kwa mwaka 2018, mauzo ya bidhaa kupitia mtandaonoi yalifikia thamani ya dola trilioni 25.6 duniani kote.

Hata hivyo katika nchi 10 zinazoongoza katika biashara hiyo hakuna hata moja kutoka mataifa machanga, mataifa hayo yakifanya biashara kati kampuni na kampuni au B2B na kampuni kwa mlaji au B2C.

Marekani imeendelea kuongoza katika biashara hiyo ya mtandaoni ikifuatiwa na China na Uingereza.

Kwa kuangalia wanunuzi wa mtandaoni, ripoti inasema kuwa katika chumi 20 za juu duniani, kiwango cha watu kutumia intaneti kununua bidhaa inatofautiana ambapo kwa mwaka huo wa 2018, asilimia 87 ya wakazi wa Uingereza walinunua bidhaa kupitia mtandaoni ikilinganishwa na Thailand asilimia 14 na India asilimia 11.

Changamoto nyingine kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadhi ya nchi haziweki takwimu sahihi za ununuzi mtandaoni na hata zinapochapisha, hazifuati kanuni za kibiashara zinazotambulika kimataifa wakati wa uchapishaji wa taarifa hizo.

Ni kwa mantiki hiyo wiki hii ya biashara mtandaoni inayoendelea hadi tarehe 1 mwezi ujao wa Mei, na kuleta pamoja kwa njia ya mtandao mawaziri, wakuu wa mashirika ya kimataifa na watendaji wakuu wa biashara na mashirika ya kiraia, utachambua mbinu sahihi za kusonga mbele baada ya Corona na kupata mbinu za kutumia vyema biashara kupitia mtandaoni.

Akizungumzia biashara ya mtandaoni na kiwango chake, Shamika Sirimanne ambaye ni Mkurugenzi wa Teknolojia UNCTAD amesema kuwa, “janga la COVID-19 limechochea utumiaji wa suluhu za kimtandao ikiwemo kupata huduma na vifaa, lakini kwa ujumla bado ni vigumu kutabiri thamani ya biashara ya mtandao kwa mwaka huu wa 2020.”