Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mwanasesere nitengenezaye ni uponyaji dhidi ya machungu niliyopitia- Mkimbizi

Mkimbizi Kituza kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akiwa kambini Maratane nchiin Msumbiji huku akiwa amebeba mwanaserere anayetengeneza na kumpatia fedha na uponyaji.
© UNHCR/Hélène Caux

Wahamiaji na Wakimbizi

Baada ya kubakwa na waasi huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na wazazi wake kuuawa kisha kupata hifadhi nchini Msumbiji, mkimbizi Kituza sasa anatumia wanasesere anaotengeneza si tu kwa kujipatia kipato bali pia kupata uponyaji na kusahau machungu aliyopitia.

Kambini Maratane, nchini Msumbiji, tunakutana na Kituza, mkimbizi huyu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Alikimbilia hapa baada ya waasi kushambulia usiku makazi yao jimboni Uvira nchini DRC na kumbaka na kuwaua wazazi wake, yeye Kituza akiwa na umri wa miaka 16.

Kambini hapa ambako ni makazi ya wakimbizi wapatao 6,000 wengi wao kutoka DRC na Burundi, Kituza anajituma kutengeneza wanasesere..

Mara ya kwanza nilitengeneza mwanasesere mmoja. Nilimpeleka katika kanisa la kikatoliki lililopo karibu na kambi na kumuonesha mtawa mmoja aitwaye Giovanna. Alipoona tu, alipenda na kuniambia nitengeneze wanasesere 160. Niliwatangeneza asubuhi hadi usiku. Nilimpelekea, alinilipa na aliwapeleka Italia.’

Kituza ambaye anasema wanasesere hufurahisha watoto alipata ujuzi kutoka kikundi cha kanisani kambini Maratane mwaka 2018 ambapo anatumia mabaki ya vitenge na kwake mradi huo ni nguzo kuu akisema,

“Napenda kazi hii, ni sehemu ya maisha yangu. Wale waliosoma ndio wanaweza kupata kazi. Kwangu mimi, kutengeneza hawa wanasesere kutanisaidia mustakabali wangu na ndio maana naifanya kwa moyo wote.”

Ndoto ya Kituza ya kupanua biashara yake inaonekana kutimizika ambapo UNHCR inasaidia wakimbizi walio hatarini na wenyeji wao Msumbiji kufanya kazi na kuanzisha miradi ili hatimaye waweze kujitegemea badala ya kutegemea misaada.

Hatua hii inamfanya Kituza afunguke zaidi akisema kuwa,

« Nimepitia machungu mengi. Imekuwa ni safari ndefu lakini sasa nikiangalia hawa wanasesere na kutambua kuwa mimi ndio nimewatengeneza, napata nafuu sana. Matumaini yangu ni kuendelea kutengeneza hawa wanasesere na kujipatia kipato.”

Suala la wakimbzi kupata kazi na kuweza kujitegemea ndio nguzo ya mkataba wa kimataifa kuhusu wakimbizi, ambao unataka kuongezwa kwa mshikamano na wakimbizi na jamii zinazowahifadhi.