Manusura wa ukatili wa kingono Sudan Kusini bado wanaishi na jinamizi:UNMISS

24 Aprili 2020

Manusura wa ukatili wa kingono nchini Sudan Kusini wengi wao bado wanaishi na jinamizi hilo wakihaha kupata huduma za msingi za afya na hata kujitenga katika jamii kutokana na unyanyapaa. 

Manusura wa ukatili wa kingono nchini Sudan Kusini wengi wao bado wanaishi na jinamizi hilo wakihaha kupata huduma za msingi za afya na hata kujitenga katika jamii kutokana na unyanyapaa. 

Katika eneo la Leer Sudan Kusini kutana na Suzanne manusura wa ukatili wa kingono  akisema wasaliti wake walikuja usiku wa mamane yeye na familia yake wakiwa wamelala na wakaanza kuwapiga mateke kuwaamsha.. Alikuwa na umri wa miaka 13 tu alipobakwa. Machozi yanambubujika akielezea jinsi gani kundi la wanaume wenye silaha walipovamia nyumba yao na kuanza kuisulubu familia yake huku wakitishia kuwapiga risasi na kumteka

“Walinikanyaga mateke na kunipiga , mmoja wao alinivuta , kuninyakua na kuondoka nami licha ya nyanya yangu kumuomba aniache. Watu nyumbani walikuwa wanapiga mayowe anirudishe . Baada ya kunifikisha kichakani alinibaka na kuniachilia  niondoke na nikaenda nyumbani peke yangu. Na nilipofika nyumbani maaskari walikuwa wamekuja wakinitafuta mimi na yeye lakini tayari nilikuwa nimeshachukuliwa na yeye ameshakimbia.”

Suzane ni miongoni mwa maelfu ya wanawake na wasichana waliopitia ukatili wa kingono wakati na baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe Sudan Kusini, alibahatika kupona baada ya kupatiwa matibabu katika kituo cha afya kisicho cha kiserikali.

Mwaka 2017 Elizabeth kama Suzane alibakwa pia lakini yeye alikuwa njiani akitembea kuelekea nyumbani Leer kwenye jimbo la Unity

“Mimi baada ya kupigwa na burutwa nikabakwa na wanaume watatu, walinikanyaka kifuani na kwenye makalio na mabuti yao , na kwa sababu ya kipigo kikubwa nilichokipata familia yangu ilitumia dawa za mitishamba kuondoa damu iliyokuwa imeganda maana nilikuwa kwenye maumivu makali ,nikapata nafuu.”

Ripoti mpya iliyotolewa na mpango wa Umoja wa Mataifa Sudan kusini UNMISS imeorodhesha changamoto nyingi ikiwemo mosi ukosefu wa huduma muhimu za afya kwa manusura wa ubakaji, pili karibu asilimia 72 ya watu wanaishi umbli wa kilometa tano kutoka kwenye kituo cha afya na tatu hakuna madaktari, wakunga na wauguzi wa kutosha wenye ujuzi  na hivyo vikwazo hivyi vya kijamii huwalazimisha manusura wengu kuteseka kimyakimya.

Kwa mujibu wa Sara Gibson afisa wa haki za binadamu wa UNMIS kuwajengea uwezo madaktari, wauguzi na wakunga inachukua muda lakini wanataka kuona serikali inatenga fungu maalum la fedha ili walibebe kwa uzito wake sula la manusura wa ukatili wa kingono kama jukumu lao la kuwapa haki ya afya.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter