Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matangazo ya elimu kwa televisheni na mtandaoni yasaidia wakimbizi Jordan

Wakimbizi wa Syria katika kambi ya Za'atari nchini Jordan.
UNICEF/Christopher Herwig
Wakimbizi wa Syria katika kambi ya Za'atari nchini Jordan.

Matangazo ya elimu kwa televisheni na mtandaoni yasaidia wakimbizi Jordan

Utamaduni na Elimu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kwa kushirikiana na serikali ya Jordan, wamechukua hatua hatua kuhakikisha kuwa wakimbizi wa Syria katika kambi ya Za’atari nchini humo wanaendelea na masomo licha ya kufungwa kwa shule 32 kambini humo kutokana na hofu ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Katika kambi hiyo kubwa zaidi ya wakimbizi eneo la Mashariki ya Kati, wanafunzi kuanzia wale wa chekechea hadi wa sekondari wanaendelea na masomo kwa njia ya mtandao kupitia televisheni au simu licha ya kwamba vifaa hivyo ni vichache.

Mafunzo yanafuata mtaala wa kitaifa wa Jordan ambapo miongoni mwa wanafunzi ni Raghad na Rania ambao baba yao Abo Ayman anatumia muda mwingi kusaidia watoto wao na ndugu zao wengine wanne kufuatilia masomo yao kwa njia ya televisheni au simu.

Baba yao mzazi Rania anasema kuwa, “nina watoto 6 ambao wanatumia simu moja kuwasiliana na makundi yao. Najaribu kutenga muda kwa kila mmoja kuungana na kundi lake, hii ina maana kwamba, wakati mwingine kuna kuchelewa katika kujibu maswali yanayotumwa na mwalimu kwenye kundi.”

Ayman na Ahmed wao ni wanafunzi wa shule ya sekondari ambao wanatumia mafunzo kupitia televisheni kuhakikisha hawakosi masomo yao.

Kwa Ayman, hakuna tofauti kubwa akisema kuwa, “ni sawa na shule ya kawaida. Hakuna kilichobadilika. Tofauti kubwa ni kwamba darasani unamuona mwalimu lakini sasa unamuona mtandaoni au kupitia televisheni.”

Hivi sasa katika kambi ya Za’atari takribani wanafunzi 18,000 wamesajiliwa kujifunza majumbani kupitia matangazo ya televisheni ya taifa.

Ili kuweza kukidhi mahitaji ya familia zilizosalia nyumbani kila siku, UNHCR na mamlaka za kambi, wameongeza usambazaji wa umeme katika kila kaya kutoka saa 8 hadi 12 kwa siku.

UNHCR inasema kuwa kwa wanafunzi wakimbizi, kwenda shule tayari ni changamoto kubwa au ni jambo lisilowezekana kwa wengi wao ambapo takwimu zinaonesha kuwa, chini ya nusu ya watoto wakimbizi wenye umri wa kwenda shule duniai kote ndio wanakwenda shule ambapo hata hivyo 1 kati ya 4 ndio anaendelea na masomo ya sekondari.

“Watoto wengi wakimbizi hivi sasa wanaweza wakawa nje ya shule kwa kipindi kirefu na baadhi yao hawatarejea kabisa,”  imesema UNHCR.

Ni kwa mantiki hiyo, baadaye wiki hii, UNHCR na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF wanatarajiwa kutoa taarifa ya pamoja kutoa wito wa kusaidia na kuelekeza zaidi msisitizo kwa ulinzi, huduma ya afya na elimu kwa watoto wakimbizi duniani kote, ili janga la COVID-19 lisitoweshe mafanikio ya awali yaliyopatikana kwa mbinde.

TAGS: Za’atari, Jordan, Syria, UNHCR