AU na Afrika wameonyesha umoja na uongozi ambao ni nadra hivi sasa kuhusu COVID-19:UN

17 Aprili 2020

Muungano wa Afrika AU na bara zima la Afrika wameonyesha umoja na uongozi vitu viwili ambavyo ni nadra sana latika nyakati hizi amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hii leo.

Antonio Guterres ametoa kauli hiyo wakati akipongeza juhudi zilizochukuliwa mapema na bara la Afrika kupambana na mlipuko wa janga la virusi vya Corona au COVID-19 kwenye mkutano ulioandaliwa na AU, shirika la fedha duniani IMF na Benki ya Dunia wa kuhamasisha na kuwasilisha ripoti ya madeni na COVID-19 uliofanyika kwa njia ya mtandao .

Guterres amesema “Tunahitaji kulenga kila nguvu tuliyonayo kuapambana na COVID-19. Tunajua kwamba virusi hivi vitasambaa kama moto wa mwituni na havina kuta za kuvikinga, na kutokana na mabadiliko ya tabianchi bara la Afrika linaweza kuishia kuathrika vibaya na janga ambalo halikulitengeneza”

Utafiti unaendelea katika kusaka chanjo na tiba ya virusi vya Corona, COVID-19
UN Photo/Loey Felipe
Utafiti unaendelea katika kusaka chanjo na tiba ya virusi vya Corona, COVID-19

COVID-19 ni zaidi ya janga la kiafya

Katibu Mkuu amesema ni bayana kuwa janga hili ni zaidi ya mgogoro wa kiafya, ni janga la ajira, janga la kibinadamu, na ni janga la maendeleo .

Na barani Afrika amesema kaya na biashara zinaathirika vibaya na changamoto za kifedha na mashinikizo mengine yaliyokuwepo hata kabla ya virusi hivi kuingia barani humo.

Janga la dharura ya maendeleo lilikumba bara hilo kabla ya janga la kiafya, lakini sasa “nchi hizo zitahitaji kupambana na vyote huku mamilioni ya waafrika wakitumbukia katika umasikini na kupoteza mamilioni ya ajira.”

Wakati huohuo amesema tayari kuna viwango visivyokubalika vya pengo la usawa, hali tete inaongezeka, bei ya bidhaa inashuka na hatua za maendeleo zilizopigwa kwa mbine sasa ziko katika tishio kubwa.

Waendesha teksi nchini Liberia wakati wa janga la Ebola mwaka 2014. Janga la COVID-19 nalo linatishia uchumi wa nchi zinazoendelea hususan za Afrika na dola bililoni 220 zinakadiriwa zitapotea.
UNDP/Morgana Wingard
Waendesha teksi nchini Liberia wakati wa janga la Ebola mwaka 2014. Janga la COVID-19 nalo linatishia uchumi wa nchi zinazoendelea hususan za Afrika na dola bililoni 220 zinakadiriwa zitapotea.

Nini cha kufanya kuisaidia Afrika

Bwana Guterres amesema ili kushughulikia athari za kiuchumi na kijamii za zahma hii tangu mwanzo amekuwa akiomba kuwepo kwa fungu la kimataifa kwa ajili ya kuinua bidhaa za jumla za pato la kimataifa.

“Kwa Afrika hii inamaanisha ni zaidi ya dola bilioni 200 na ili kuzifikia ni lazima tuchagize washirika wote. Napongeza hatua za IMF na Benki ya Dunia kuzisaidia nchi wanachama na ahadi ya kuimarisha furs ana nyezo muhimu.”

Hata hivyo Katibu mkuu amesema “tunahitaji rasilimali kubwa zaidi kwa IMF Pamoja na utoaji wa haki maalum za uchukuaji fedha zaidi na msaada ulioimarishwa kwa Benki ya Dunia, mifumo na taasisi zingine za kimatifa za fedha. Lakini kupunguza madeni ni muhimu sana, ninakaribisha hatua za G-20 zikiwemo kusitisha ulipaji wa madeni kwa nchi zote za IDA na nchi zinazoendelea.”

Guterres amesema huo ni mwanzo lakini hali halisi inahitaji hatua zaidi ya hizo akisema nchi nyingi zinazoendelea ziko katika hali mbaya na zinalemewa na mzigo wa madeni au zitajikuta na mzogo wa madeni kutokana na mdororo wa kiuchumi.

“Barani Afrika wastani wa madeni kwa pato la taifa GDP umeongezeka kutoka asilimia 39.5 mwaka 2011 na kufikia asilimia 61.3 mwaka 2019.”

Kunahitajika mfumo maalum wa kushughulikia madeni

Katibu Mkuu amesema kunahitajika kuwa na mfumo unaojitosheleza na wa kina kuhusu masuala ya madeni na ambao ni wa awamu tatu.

Mosi- Kusitisha madeni yote kwa nchi zinazoendelea ambazo hazina fursa ya masoko ya fedha na haziwezi kulipa madeni yao.

Pili-kuwepo na chaguo zaidi la madeni endelevu kwa mifumo kama kubadilishana madeni na kuwa na mfumo wa madeni kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Tatu-Kushughulikia masuala ya kimuundo katika madeni ya kimataifa kuzuia watu kutumbukia katika mgogoro wa madeni wa muda mrefu kwa kushindwa kulipa. Ni lazima kujikita na wasiojiweza na kuhakikisha kwamba haki za watu wote zinalindwa.

Katibu Mkuu amesema hii inamaanisha kujikita na athari za virusi hivi kwa Watoto, watu wenye ulemavu na makundi mengine yaliyo hatarini.

Mshikamano unahitajika kushinda COVID-19

Hatimaye Katibu Mkuu amesema wanafanyafazi kwa karibu na shirika la afya duniani WHO na wengine katika kuunda mshikamano wa kimataifa kusongesha mbele juhudi za chanjo haraka iwezekanavyo.

“Ujumbe wangu ni huu, kwamba chanjo lazima ipatikane na kuwa na gharama nafuu kwa kila mtu kila mahali.”

Amesisitiza kwamba “Wakati maalum unahitaji mshikamano maalum. Moja ya mtihani muhimu wa mshikamano wa kimataifa ni kushikamana na Afrika kwa ajili ya mafanikio ya bara hilo na dunia. Nitaendelea kuhamasiha na kuhimiza wito wa viongozi wengi wa Afrika ambao wamesema ushindi barani Afrika ndio utakaomaliza mlipuko huu kila mahali.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter