Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuko watu tisa katika chumba kimoja, tunaihofia COVID-19- Qusai Al-Khatib

Wakimbizi wa ndani nchini Syria waliokimbia machafuko kusini mwa Idlib na mashariki mwa Aleppo.
© UNICEF/Khaled Akacha
Wakimbizi wa ndani nchini Syria waliokimbia machafuko kusini mwa Idlib na mashariki mwa Aleppo.

Tuko watu tisa katika chumba kimoja, tunaihofia COVID-19- Qusai Al-Khatib

Afya

Wakati janga la COVID-19 likiendelea kuuzingira  ulimwengu, familia za raia wa Syria zilizoko hatarini zina hofu zaidi kwa sababu zinaendelea kuishi katika mazingira yenye msongamano mkubwa na kukiwa na nafasi finyu ya kupata huduma za afya.

Hii ni kambi ya Barisha wanamoishi wakimbizi wa ndani wa ndani wa Syria katika eneo la Idlib. Mwanamama Qusai Al-Khatib ni mmoja wa wakimbizi wa ndani wanaoishi kambini hapa anaonekana akiosha vyombo, kisha akimvalisha nguo mtoto na baadaye akinywa kahawa na watoto wakiwa wamekaa sakafuni. Bi Al-Khatib anasema,“Nina chumba kimoja na watoto wangu, na binti yangu ana watoto wawili. Tuko watu tisa katika chumba kimoja. Tunakabiliana na shida nyingi mahali hapa.”

Qusai Al-Khatib ni mjane ambaye alifurushwa kutoka Kfar Nabl kwenye jimbo la Idlib wakati mashambulizi ya mabomu yalipoongezeka katika mji wao. Pamoja na watoto wake saba na wajukuu wawili, wamekuwa wakiishi katika kambi hiyo ya wakimbizi wa ndani kwa zaidi ya miezi kumi sasa.  Sasa mama huyu ana hofu juu ya maisha yao ikiwa ugonjwa wa COVID-19 utaingia katika kambi yao,“Virusi vya corona vimesambaa duniani kote tuna hofu kuhusu hilo. Tunaogopa kwasababu kuna idadi kubwa ya watu hapa kwenye kambi na mara zote tunakutana. Maji yetu ni ya pamoja. Chakula chetu ni cha kushirikiana. Mkate wetu ni wa pamoja. Mahema yamekaribiana. Tunaogopa sana janga hili linaweza kusambaa hapa.”

Qusai anasema anafanya kila anachoweza ili kufanya virusi vya corona visiwafikie. Anasema anakuwa na hofu mara zote watoto anawaosha na sabuni na maji wanaporejea kutoka nje kucheza, lakini ana hofu kwa kuwa maji si ya kutosha kambini na hayatoki mara kwa mara.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA, inashirikiana na wadau wake muda wote kupunguza hatari za COVID-19, lakini rasilimali zaidi zinahitaji haraka.