Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi DRC hawaamini kuwa Ebola imeibuka tena- WHO

Wafanyakazi wa kituo cha Ebola cha Katwa Butembo, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC wakisafisha viatu na nguo
UN Photo/Martine Perret
Wafanyakazi wa kituo cha Ebola cha Katwa Butembo, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC wakisafisha viatu na nguo

Wananchi DRC hawaamini kuwa Ebola imeibuka tena- WHO

Afya

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako wagonjwa wapya  wanne wa Ebola wamebainika tangu tarehe 10 mwezi huu wa Aprili, watoa huduma wanaelezea kile ambacho wanakabiliana nacho katika kupambana na mlipuko huu wakati huu ambapo taifa hilo la Maziwa Makuu pia linakabiliwa na ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19 na machafuko katika baadhi ya majimbo

Ijumaa iliyopita ya tarehe 10 mwezi huu wa Aprili, shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, lilikuwa linajiandaa kutangaza kuwa Ebola imetokomezwa nchini DRC baada ya kukamilika kwa siku 54 bila kuwepo kwa mgonjwa mpya. Hata hivyo siku hiyo hiyo mgonjwa mpya akabainika na hadi sasa idadi imefikia wanne na wagonjwa wawili wamefariki dunia.

Watoa huduma dhidi ya Ebola wanasema juhudi zao za kudhibiti gonjwa hilo zinakumbwa na vikwazo ikiwemo ukosefu wa usalama na wananchi kutoamini kuwepo kwa Ebola.

Abdourahmane Diallo, afisa wa WHO anayeongoza mpango wa chanjo dhidi ya Ebola nchini DRC ansema kuwa kwa bahati mbaya wamekuwa wakikumbwa na upizani mkubwa juu ya wagonjwa hao wapya.

Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, Bwana Diallo amesema kuwa jamii haiamini ya kwamba kuna wagonjwa wapya wa Ebola, hali inayowapa mkwamo mkubwa wafanyakazi watoa huduma mashinani.

Hata hivyo amesema wanajitahidi kwa kadri ya uwezo wao kuwasiliana na wananchi na kuwashawishi ili mtu yeyote aliyekuwa ameambatana au kuwa karibu na wagonjwa wapya ajitokeze ili apatiwe chanjo dhidi ya Ebola.

Bwana Diallo anasema kuwa matarajio yao yalikuwa kufunga vituo vya matibabu ya Ebola lakini kutokana na wagonjwa wapya wa Ebola sambamba na wale wa COVID-19 vituo hivyo vitaendelea kuwa wazi.

Amesema licha ya vikwazo bado wana ari kubwa ya kuendelea na kazi na wanatumia mbinu mbalimbali kushawishi wananchi, ikiwemo mbinu bora za mawasiliano na jamii kama vile ujumbe wanaopeleka kutoka WHO uwe ni mmoja na sahihi,  mavazi yao yanakuwa ya kawaida ili kufanana na wananchi.

Hadi sasa DRC imeripoti wagonjwa 267 wa COVID-19 ambapo kati yao hao 22 wamefariki dunia.