Watoto wako katika hatari zaidi ya kuathiriwa na muda mwingi mitandaoni wakati huu wa COVID-19-UNICEF

15 Aprili 2020

Mamilioni ya watoto wako hatarini kudhurika wakati huu ambao maisha yao yamehamia zaidi mitandaoni wakati wa kukaa ndani kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19, imeeleza taarifa iliyotolewa hii leo mjini New York Marekani na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF pamoja na wadau wake.

UNICEF na wadau wake ambao ni Global Partnership to End Violence Against Children ambayo ni taasisi ya kutokomeza unyanyasaji dhidi ya watoto, shirika la kimataifa la muungano wa mawasiliano, ITU, Shirika la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na madawa na uhalifu UNODC, WHO, WePROTECT Global Alliance na World Childhood Foundation wametoa waraka unaolenga kuzisihi serikali, tasnia ya mawasiliano, watoa elimu pamoja na wazazi kuwa makini na kuchukua hatua za kupunguza hatari na kuhakikisha uzoefu wa watoto mitandaoni unakuwa salama na unatoa mchango chanya wakati huu wa COVID-19.

Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF Henrietta Fore amesema, “katika kivuli cha COVID-19, maisha ya mamilioni ya watoto kwa muda yamejikita katika nyumba zao na vifaa vyao vya kielekroniki. Tunatakiwa kuwasaidia kupita katika ukweli huu mpya. Tunatoa wito kwa serikali na tasnia kuunganisha nguvu kuwaweka watoto salama mitandaoni kupitia huduma zilizoboreshwa na zana mpya za kuwasaidia wazazi na watoa elimu kuwafundisha watoto wao jinsi ya kutumia intaneti kwa usalama.”

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Global Partnership to End Violence akilisisitiza suala hilo anasema, “kusambaa kwa virusi cha corona kumesababisha kuongezeka kwa kasi kwa muda wa kuangalia vifaa vya kielekroniki. Kufungwa kwa shule pamoja na hatua kali za kuudhibiti ugonjwa vinamaanisha familia kutegemea zaidi kwenye teknolojia na dijitali ili kuwafanya watoto wajifunze, kuburudika na kuungana na watu waliko nje ya mazingira yao, lakini si wote wana uelewa, ujuzi na rasilimali za kujiweka salama wawapo mitandaoni.”

Taarifa hiyo ya UNICEF inaendelea kusema kuwa zaidi ya watoto na watu bilioni 1.5 pamoja na watu wengine wa umri mdogo wameathirika na kufungwa kwa shule duniani kote. Wengi wa wanafunzi hawa hivi sasa wanapata mafunzo yao pamoja na kuwasiliana na wenzao kupitia mitandaoni. 

“Kutumia muda mwingi katika mitandao kunaweza kuwaweka watoto katika hatari ya  manyanyaso ya kingono pamoja na kuingizwa katika tabia hizo kwani watu wabaya wanataka kutumia janga hili la COVID-19 kutekeleza mambo mabaya.” Imeeleza taarifa hiyo ya UNICEF.

Aidha taarifa hiyo imesema kukosekana kwa fursa ya watoto kukutana ana kwa ana na marafiki na wenzi wao kunaweza kusababisha hatari ya watoto kutumiana picha chafu na pia muda mwingi wa kukaa mtandaoni unaweza kuwafanya watazame maudhui ya vurugu na pia kuwaweka katika uwezekano wa kufanyiwa manyanyaso mtandaoni. 

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter