Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa Mwangaza Mashinani Kenya waua ndege wawili kwa jiwe moja

Wakazi wa mpakani Kenya na Uganda nchini Kenya.
WFP
Wakazi wa mpakani Kenya na Uganda nchini Kenya.

Mradi wa Mwangaza Mashinani Kenya waua ndege wawili kwa jiwe moja

Msaada wa Kibinadamu

Nchini Kenya, mradi wa pamoja kati ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF na wadau wake wa kupatia nishati ya sola kwa wakazi wenye kipato duni vijijini umekuwa ni sawa na kauli ya wahenga wa jiwe moja kuua ndege wawili badala ya ndege mmoja kama ilivyotarajiwa hapo awali.

Ni katika kaunti ya Baringo nchini Kenya, moja ya maeneo ambako mradi wa Mwangaza Mashinani unatekelezwa kwa lengo la kuongeza muda wa watoto kusoma usiku kwa kutumia taa za sola ambazo kaya zao zimepatiwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF pamoja na wadau wake.

Susan Momanyi, afisa wa UNICEF Kenya anafunga safari kukagua ufanisi wa mradi nyumbani kwa Regina John, mmoja wa wanufaika ambaye ni mama wa watoto watatu, akiwemo Purity ambaye aliugua homa ya uti wa mgongo.

Punde wanafika kwa Regina ambaye anazungumzia faida za taa za sola kwa masomo ya wanae.“Hapo awali kabla sijapata hicho kifaa, nilikuwa napitia hali ngumu hasa upande wa watoto kusoma watoto pale ndani. Walikuwa hawawezi kusoma nyakati za usiku kwa sababu nilikuwa natumia lile taa la mkopo ambalo lina moshi mkali. Wakati alikuwa hajapata hicho kifaa alama zake zilikuwa ziko chini sana. Saa hii anasoma vizuri na alama zake zimepanda, alikuwa na D+ sasa anapata na B+.”

Na kisha akaelezea ni kwa vipi mradi ulimgusa pia Purity ambaye ameshapona na ameanza tena masomo..“Na hizo dawa zilikuwa kila baada ya saa 5 umpatie dawa, kila baada ya saa 5 umpatie dawa, na hivyo ulinisaidia sana kwa sababu nilikuwa namwangilia usiku kucha, siwezi ati kutafuta taa kwa sababu hakuna taa. Hilo taa lilkuwa linawaka usiku mzima nikiangalia huyo mtoto.”

Susan anasema wao UNICEF wanakusanya ushahidi kuona ni kwa vipi mradi huu wa sola unaweza kufikia kaya zenye kipato cha chini zaidi na hata kuongeza muda wa malipo ya vifaa vya sola.  Na zaidi ya yote,“Unaona mabadiliko, unaona jinsi ambavyo tunabadilisha maisha, unaona ni jinsi gani tunainua familia, na hii ni furaha ya kipekee.”

Wadau wengine kwenye mradi huo ni serikali ya Kenya, ubalozi wa Sweden nchini Kenya na Energy 4 Impact.