Mlipuko wa COVID-19 haujakwamisha harakati za FAO na serikali ya Kenya kudhibiti nzige wa jangwani

Kundi la nzige likiwa angani kwenye moja ya mashamba
© FAO/Giampiero Diana
Kundi la nzige likiwa angani kwenye moja ya mashamba

Mlipuko wa COVID-19 haujakwamisha harakati za FAO na serikali ya Kenya kudhibiti nzige wa jangwani

Masuala ya UM

Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, linaendelea na juhudi za kudhibiti baa la nzige wa jangwani katika nchi za Afrika Mashariki licha ya vikwazo vya kusafirisha watendaji na vifaa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19.

Baa la nzige limeendelea kuwa tishio hususan Ethiopia, Kenya na Somalia ambako wadudu hao waharibifu wanatishia usalama wa chakula na mbinu za wananchi kujipatia kipato.

Taarifa ya FAO iliyotolewa leo mjini Roma, Italia, makao makuu ya shirika hilo, imesema kuwa takribani watu milioni 20 wanaathiriwa na uwepo wa wadudu hao katika nchi za Ethiopia, Kenya Somalia, Sudan Kusini na Uganda pamoja na watu wengine milioni 15 nchini Yemen ambako pia wadudu hao wamevamia.

FAO inasema mvua kubwa za mwezi uliopita zinatarajiwa kuchochea ongezeko la wadudu hao eneo la Afrika Mashariki katika miezi ijayo huku wengine wakitatarajiwa kusafiri kutoka Kenya hadi Sudan Kusini na Uganda.

Hali nayo ni tete Iran na Yemen ambako nzige hao wa jangwani wameshuhudiwa.

Licha ya vikwazo tunashirikiana na serikali kubuni mbinu mpya

Kiongozi wa timu ya FAO inayohusika na ufuatiliaji na udhibiti wa nzige hao, Cyril Ferrand amesema kuwa, “vizuizi vya safari kutokana na COVID-19 vimekuwa ni changamoto kubwa katika safari za watendaji na usafirishaji wa vifaa lakini FAO inaendelea kushirikiana na serikali husika, wakulima ili kudhibiti mlipuko.”

Amesema hakuna dalili zozote za kupungua kwa nzige hao kwa sababu maeneo yote ambayo yameathirika, na kwamba ingawa karantini sasa ni hali halisi, watu wanashiriki katika vita dhidi ya nzige hao kwa kuwa wanaruhusiwa kufanya ufuatiliaji kwa njia ya anga na ardhini.

Inachofanya FAO ni kuimarisha juhudi za serikali kwa kuzipatia vifaa vya ufuatiliaji ambapo upulizaji wa dawa unafanyika ardhini na kutokea angani katika nchi 10.

Hadi sasa zaidi ekari 240,000 zmepuliziwa dawa ya kuua nzige katika eneo hilo la Afrika Mashariki na watu 740 wamepatiwa mafunzo ya kudhibiti nzige kutokea ardhini lakini COVID-19 imeleta mkwamo katika upatikanaji wa mashine zenye mota za kupulizia dawa pamoja na dawa zenyewe za kuua wadudu.

Akifafanua mkwamo huo, Bwana Ferrand amesema, “changamoto kubwa sasa ni kupata dawa za kuulia watutu kwa sababu safari za ndege za mizigo zimepungua kwa kiasi kikubwa. Kipaumbele chetu sasa ni kuzuia kupungua kwa dawa hizo katika kila nchi. Iwapo hilo litatokea basi itakuwa ni pigo kubwa kwa wakazi wa vijijini ambao tegemeo lao ni mafanikio ya kampeni dhidi ya nzige ili wapate chakula na njia za kujipatia kipato.”

Kwa kuwa COVID-19 imesababisha karantini, na hivyo watendaji wa FAO na wadau wao kushindwa kufanya operesheni za ufuatiliaji, FAO imeimarisha ukusanyaji wa data kwa mtandao ikisema kuwa mtandao wa wadau, mashirika ya kiraia, maafisa ugani na mashirika ya mashinani ni muhimu katika kupata data sahihi kutoka maeneo mbali mbali hususan Kenya, Somalia, Ethiopia na Sudan Kusini.