Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Rais wa Baraza Kuu la UN Tijjani Muhammad-Bande (kushoto) na mkuu wake wa utawala Balozi Mari Skåre, wakati wa kikao kilichofanyika kwa mtandao na nchi wanachama 27/3/2020

COVID-19 ikiendelea Baraza Kuu la UN linakutana vipi?

OPGA74
Rais wa Baraza Kuu la UN Tijjani Muhammad-Bande (kushoto) na mkuu wake wa utawala Balozi Mari Skåre, wakati wa kikao kilichofanyika kwa mtandao na nchi wanachama 27/3/2020

COVID-19 ikiendelea Baraza Kuu la UN linakutana vipi?

Masuala ya UM

Ijapokuwa yaonekana kuwa dunia nzima iko kwenye karantini ikiwa ni masharti ya kiafya ili kuepuka kusambaza virusi vya ugonjwa wa Corona au COVID-19, vikao vya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwenye makao makuu ya chombo hicho chenye wanachama 193 vinaendelea, kwa kutumia teknolojia.

Huo ni ujumbe kutoka kwa Balozi Mari Skåre, mkuu wa masuala ya utawala kutoka ofisi ya Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ujumbe alioutoa akizungumzia ni kwa vipi janga lililokumba dunia hivi sasa limebadili kanuni za utendaji za chombo hicho chenye uwakilishi mkubwa zaidi duniani.

“Tulipotambua ya kwamba kuwa janga hilo ni suala la afya ya umma hapa jijini New York, Marekani, tulichukua hatua haraka na kuanza kuahirisha vikao vya uso kwa uso,”  amesema Balozi Skåre kutoka Norway alipohojiwa na UNNews.
Amesema kuwa Baraza Kuu ni jukwaa lenye uwakilishi mkubwa zaidi duniani ambako nchi wanachama wanakutana na kupitisha maamuzi, ni kama jukwaa la mjadala la dunia nzima, “kwa hiyo tulitaka kuhakikisha kuwa maamuzi hayo yanaweza kuendelea. Na kwa hiyo basi mbinu tulizochagua zilikuwa iwe kwa maandishi lakini pia kupitia mikutano kwa njia ya video.”

Balozi Mari Skåre, Mkuu wa utawala Ofisi ya Rais wa Baraza Kuu la UN akiwa ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu.
OPGA74
Balozi Mari Skåre, Mkuu wa utawala Ofisi ya Rais wa Baraza Kuu la UN akiwa ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu.

COVID-19: Mabadiliko na Kufutwa kwa Vikao

Watu wengi wanafahamu kuhusu Baraza Kuu kutokana na wiki yake ya vikao vya ngazi ya juu vinavyofanyika mwezi Septemba, vikao ambayo huleta pamoja viongozi na wakuu wan chi 193 wanachama wa Umoa wa Mataifa.
Baraza Kuu ni ambako nchi zote zinapaza sauti zao, na ni miongoni mwa vyombo vikuu 6 vya Umoja wa Mataifa. Vingine ni Sekretarieti, Baraza la Kiuchumi na Kijamii au ECOSOC, Baraza la Wadhamini, Baraza la Usalama na Mahakama ya Kimataifa ya Haki au ICJ.

Mabalozi wawakilishi wa nchi wanachama hukutana katika ukumbi wa kipekee kwa ajili ya mikutano ya masuala mbalimbali kuhusu maendeleo, amani, au mengine kwa mujibu wa Chata ya Umoja wa Mataifa. Halikadhalika hupigia kura maazimio na maamuzi, ambapo matokeo ya kura huonyeshwa kwenye skrini kubwa ukumbini.
Wakati huu sasa amri ya kutochangamana imetangazwa ni jambo la kila mtu, mikutano kadhaa imeahirishwa au imefutwa, kama vile kumbukizi ya mauaji ya kimbari Rwanda iliyokuwa ifanyike tarehe 7 mwezi Aprili.


Kanuni ya ukimya

Baraza Kuu hata hivyo imeendelea kupitisha maazimio na maamuzi wakati huu wa janga la COVID-19.
Bi. Skåre amesema kuwa kadri hali ilivyobadilika, nchi zilizidi kuaminiana na kwa mara ya kwanza ziliidhinisha kile alichoeleza Bi. Skåre  kuwa ni kanuni ya muda mfupi na isiyo ya kawaida kabisa.
Rais wa Baraza Kuu Tijjani Muhammad-Bande, sasa anasambaza kwa wanachama kwa njia ya mtandao rasimu ya maazimio kupitia kile kiitwacho, kanuni ya ukimya.  Mabalozi wanapatiwa ukomo wa saa 72 za kupitia, kushauriana na serikali zao, kama ni lazima, kabla ya kuelezea uamuzi au maoni yao.

Azimio litakuwa limepitishwa iwapo hakuna upinzani wowote na Rais atasambaza barua ya kuthibitisha kupitishwa kwa azimio husika.Hata hivyo litakuwa limevurugika iwapo nchi moja itapinga na Rais atajulisha mabalozi kuwa kanuni ya ukimya imevunjwa.

Bi. Skåre ameeleza kuwa katika mazingira ya kawaida, Baraza Kuu hupigia kura azimio iwapo nchi mwanachama atataka hivyo lakini hivi sasa hilo kiufundi haliwezekani.
“Katika mazingira ya sasa hatuna kanuni zozote za upigaji kura. Tunazidi kutafiti na pia tutajadili na nchi wanachama na kushauriana kwa sababu kunaweza kukawepo na maoni tofauti iwapo hilo ni lazima au la,"  amesema Bi. Skåre.

Ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
UN Photo/Amanda Voisard
Ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa


Kazi muhimu zinaendelea


Tangu kuanza kutekelezwa kwa kanuni ya ukimya, Baraza Kuu limepitisha maazimio kadhaa, ikiwemo lile la kuchangia ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika huko Darfur, Sudan, UNAMID na pia azimio kuhusu COVID-19.
Azimio hilo lilifuatia mkutano kuhusu janga hilo ambapo Rais wa Baraza Ku una viongozi wengine wa vyombo vikuu vya Umoja wa Mataifa walikuwa na mkutano na nchi wanachama kwa njia ya video.

Akizungumza kwa niaba ya sekretarieti ya Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa umoja huo, António Guterres aliwahakikishia mabalozi kuwa kazi muhimu itaendelea bila rabsha zozote.

Bi. Skåre na wafanyakazi wa ofisi ya Rais wa Baraza Kuu nao pia hawajashuhudia kupungua kwa kazi. Wafanyakazi wote wanafanyia kazi kutokea nyumbani na vikao vya watendaji wa ofisi hiyo vinafanyika kwa njia ya mtandao, ingawa siku moja moja baadhi wanakwenda ofisini ili kurahisisha utendaji.

Katu tusimwache mtu nyuma

Kwa kwa alishakuwa Balozi wa Norway nchini Afghanistan, Bi. Skåre anazingatia hali ilivyo ya majanga nchini humo na COVID-19. Katika mazingira yote anahakikisha kuendelea kwa kazi ni muhimu kwa kuangazia usalama wa wafanyakazi, uratibu na kufikia wananchi mashinani.

“Janga hili ni mshtuko mkubwa kwa jamii na chumi zetu. Tunahitaji kuangalia mbali zaidi kuliko kile kinachotokea hivi sasa kwenye jamii zetu na kuanza kupanga jinsi ya kupunguza athari za kiuchumi,” amesema Balozi huyo.

Kwa Bi. Skåre, kukwamuka ni ahadi ya kutomwacha yeyote nyuma, kama ambavyo nchi wanchama wa Umoja wa Mataifa zimeahidi pindi zilipopitisha ajenda 2030 ya maendeleo endelevu wakati wa mkutano wake wa ngazi ya juu mwaka 2015.

Ametumia mahojiano na UNNews kuelezea hofu yake kuwa janga la Corona linaweza kurudisha nyumba haki za wanawake, hasa kwa kuzingatia kuwa mwaka huu ni miaka 25 tangu azimio la ulingo wa Beijing.

“Tumesonga kama jamii ya kimataifa lakini wanawake hawapo. Hawashiriki ipasavyo kwenye maendeleo ya kiuchumi, soko la ajira, biashara na kupitisha maamuzi kama ilivyo kwa wanaume na kuna hatari kubwa ya kwamba janga la Corona linaweza kuengua wanawake kutoka soko la ajira na maendeleo ya kiuchumi,”  alisema.
 

Amesisitiza kuwa katu tusikubali hilo litokeaa, “tusiruhusu vikwazo katika kuongeza ushiriki wa wanawake. Hiki ni kitu muhimu sana kwangu na ni ujumbe muhimmu kwa kila mtu anayepanga mipango yooyte hivi sasa.”