Kitabu cha watoto chazinduliwa kuwaelimisha kuhusu COVID-19

9 Aprili 2020

Zaidi ya mashirika 50 ya kibinadamu yakiwemo yale ya Umoja wa Mataifa yameandaa kitabu kipya cha kusaidia watoto kuelewa na kufahamu kwa kina ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la afya, WHO, la kuhudumia watoto, UNICEF, la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na lile la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO na wadau wao likiwemo Save the Children na shirikisho la vyama vya  nyekundu na hilal nyekundu.
Kwa msaada wa kikaragosi cha kufikirika, Ario, kitabu  hicho kiitwacho “Shujaa wangu ni Wewe, Jinsi gani watoto wanaweza kupambana na COVID-19 kinaeleza ni kwa vipi watoto wanaweza kujilinda wenyewe, familia zao na marafiki dhidi ya virusi vya Corona na ni kwa vipi wanaweza kukabili hisia pindi wanapokumbana na hali halisi inayobadilika haraka na mara kwa mara.
Walengwa ni watoto wenye umri wa kuanzia miaka 6 hadi 11 na ni mradi wa kamati ya mashirika mbalimbali kuhusu afya ya akili na usaidizi wa kisaikolojia katika mazingira ya dharura.

Mwanzoni mwa maandalizi ya kitabu hicho, zaidi ya watu 17000 wakiwemo watoto, wazazi, walezi na walimu kutoka kona mbalimbali duniani walielezea jinsi gani wanakabiliana na janga la COVID-19.
Michango  yao ilikuwa muhimu kwa mwandishi wa kitabu na mchoraji Helen Patuck na timu nzima katika kuhakikisha simulizi na ujumbe vinaendana na watoto wa hali tofauti na maeneo mbalimbali duniani.

Wakuu wa Mashirika husika wazungumza

Akizungumzia kitabu hicho, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus, amesema, “majanga ya awali ya kibinadamu yametuonesha ni jinsi gani muhimu kushugulikia hofu na wasiwasi wa vijana pindi maisha waliyoyazoea yanapobadilika. Tunatumaini kitabu hiki chenye picha kinachosafirisha watoto maeneo mbalimbali duniani kitasaidia waelewe kile wanachoweza kufanya na kuwa na mtazamo chanya na kuwa salama wakati wa mlipuko wa COVID-19.”

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore, amesema kuwa duniani kote, maisha ya watoto yamebadilika, wengi wao katika nchi zenye karantini na hivyo, “kitabu hiki kitasaidia watoto kuelewa na kukabiliana na hali ya sasa na kujifunza ni kwa vipi wanaweza kuchukua hatua ndogo tu na kuwa mashujaa katika simulizi zao.”

Ili kuhakikisha kitabu hicho kinafikia watoto wengi kadri iwezekanavyo, kitatafsiriwa kwa lugha nyingi, ambapo leo kitabu hicho kitazinduliwa kikiwa katika lugha 6 huku nyingine 30 zikiwa kwenye maandalizi. 

Kitabu kinaweza kusomwa kwa maandishi kwenye mtandao na pia kusikilizwa kwa sauti kwenye intaneti.
Ugonjwa wa virusi vya Corona ulitangazwa dharura ya afya ya binadamu mwezi Januari mwaka huu na hadi sasa umeshasambaa katika nchi 212 duniani kote na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 79 385 kati ya wagonjwa 1,356,780.

Kupakua kitabu hicho katika mfumo wa PDF kwa lugha ya kiingereza bofya hapa.
 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter