Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yajipanga mapema kudhibiti COVID-19 katika kambi za wakimbizi wa Rohingya

Watoto wakimbizi wa Rohingya wakionekana wakipitia katika maji baada ya mvua kunyesha katika makazi yao ya muda Cox's Bazar Bangladesh
UNICEF/UN0213967/Sokol
Watoto wakimbizi wa Rohingya wakionekana wakipitia katika maji baada ya mvua kunyesha katika makazi yao ya muda Cox's Bazar Bangladesh

UNHCR yajipanga mapema kudhibiti COVID-19 katika kambi za wakimbizi wa Rohingya

Wahamiaji na Wakimbizi

Pamoja na kuwa hakuna mgonjwa yeyote wa virusi vya corona, COVID-19 ambaye ameripotiwa miongoni mwa wakimbizi nchini Bangladesh, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR linachukua hatua za kujiandaa kukabiliana na mlipuko ikiwemo kujenga wodi za kuwatibu wagonjwa katika maeneo hayo. 

Mwakilishi wa UNHCR nchini Bangladesh Steven Corliss akizungumza katika kituo cha tiba kinachojengwa katika eneo la Ukhiya ili kiwahudumie wakimbizi wa Rohingya na jamii wenyeji katika wilaya ya Cox’s Bazar amesema, “mpaka sasa, ni kama tumekuwa na bahati hakuna mgonjwa wa COVID-19 katika makazi ya wakimbizi wa Rohingya kusini mwa Bangladesh lakini tuko katika mbio dhidi ya muda. Tunajaribu kuwa tayari lakini unaona nyuma yangu kuna kituo cha kuwatenga na kuwatibu wagonjwa ambacho kinaweza kutoa huduma ya haraka kwa watu 150 hadi 200.”

Aidha Bwana Corliss anaendelea kusema, “vituo kama hivyo vinajengwa katika maeneo tofauti ndani na pia maeneo karibu na makazi ya wakimbizi wa Rohingya. Vituo hivyo vitawahudumia wakimbizi lakini vitawahudumia jamii za wenyeji. Hii ni muhimu, virusi haviangalii hadhi yako, haijalishi kama wewe ni mrohingya au mbangladeshi kwa hivyo kila kitu tunachokifanya, kila hatua zetu lazima ziwe kwa ajili ya jamii zote mbili. Umoja wa Mataifa na wadau wetu mashirika yasiyo ya kiserikali wanafanya kazi kwa ukaribu sana na serikali kuhkikisha kuwa kunakuwa na mipango hiyo.”

 

Serikali ya Bangladeshi, ikiongoza katika mapambano dhidi ya COVID-19, imeweka mpango wa kitaifa ambao unawazingatia wakimbizi. Jumuiya ya misaada ya kibinadamu inaendelea kuhakikisha kuwa wakimbizi wanajumuishwa ipasavyo katika kutekeleza mipango hii. Zaidi, UNHCR na taasisi nyingine za kibinadamu zimekamilisha mpango wa sekta mbalimbali na sekta ya afya katika Cox’s Bazar ili kuiunga mkono serikali.

Kumefanyika mafunzo ya kukinga ugonjwa kwa wafanyakazi wa sekta ya afya na pia uhamasishaji wa utaratibu wa kujisafi. 

Zaidi ya wahudumu wa afya wakimbizi wanaojitolea wapatao 1400 wanafanya kazi katika kambi ili kuhakikisha ujumbe muhimu unawafikia jamii ya wakimbizi.