Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 ina athari kubwa katika saa za kufanyakazi na mapato duniani:ILO

Wauguzi na wahudumu wa afya wakiwa nje ya hospitali jijni New York wakitaka ulinzi zaidi dhidi ya COVID-19
Giles Clarke
Wauguzi na wahudumu wa afya wakiwa nje ya hospitali jijni New York wakitaka ulinzi zaidi dhidi ya COVID-19

COVID-19 ina athari kubwa katika saa za kufanyakazi na mapato duniani:ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Mlipuko wa virusi vya Corona au COVID-19 umeelezwa kuwa na athari mbaya katika saa za kufanya kazi na mapato kote duniani kwa mujibu wa ripoti mpya iliyotolewa na shirika la kazi duniani ILO ambaye inaainisha kanda na sekta zilizoathirika zaidi na kupendekeza sera za kukabiliana na mgogoro huu wa kimataifa.

Ripoti hiyo ya ILO inasema janga la COVID-19 linatarajiwa kufuta asilimia 6.7 ya saa za kazi kote duniani katika robo ya pili ya mwaka 2020 sawa na wafanyakazi wanaofanya kazi kwa siku nzima milioni 195 .

Akizungumzia hali hiyo mkurugenzi mkuu wa shirika la ILO Guy Ryder amesema “Tangu ILO ilipotoa makadirio ya kwanza ya athari za janga hili katika ajira mnamo Machi 18, mengii yametokea. Virusi vya COVID-19 vimesambaa duniani kote, nchi nyingi zimechukua hatua ya kufunga kila kitu au sehemu kubwa ya shughuli zote kwa kiwango ambacho sasa wafanyakazi 4 kati ya 5 duniani wanaishi katika nchi ambako kila kitu kimesitishwa na watu wanasalia majumbani.

Nchi zilizoathirika zaidi

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya ILO punguzo kubwa la saa za kufanya kazi linashuhudiwa katika mataifa ya nchi za Kiarabu ambako ni asilimia 8.1 sawa na wafanyakazi milioni 5 wa kutwa nzima, ikifuatiwa na Ulaya asilimia 7.8 au wafanyakazi wa kutwa nzima milioni 12, Asia na Pasifiki zote zikiwa katika asilimia 7.2 sawa na wafanyakazi wa kutwa nzima milioni 125.

Hasara kubwa inatarajiwa katika makundi mbalimbali ya vipato lakini hususan katika nchi za kipato cha juu na cha wastani. Hali hii imepita sana ile iliyojitokeza kati yam waka 2008 -2009 wakati wa mdororo wa kiuchumi.

Sekta zilizoathirika zaidi

Kwa mujibu wa mkurugnezi wa ILO “Kuna sekta 4 ambazo ziko hatarini zaidi  ambazo ni biashara ya jumla na rejareja,  huduma na biashara ya chakula, uongozi na uzalishaji au viwanda, nah apo ndipo tulipo sasa. Hizi ni za muda mfupi lakini athari za sasa ni kuwaumiza watu kwa kishindo na kwa haraka.”

Na kuhusu idadi hii ya kupotea kwa ajira itakuwaje hapo baadaye bwana Ryder amesema “ni vigumu kujua tutakuwa wapi mwishoni mwa mwaka huu na hatujaribu kutabiri idadi ya wapi tutakapokuwa mwishoni mwa mwaka huu.”

Ameongeza kuwa hali itategemeana na mambo makuu mawili “Mosi ni jinsi gani jumuiya ya kimataifa itakavyofanikiwa kudhibiti na kuushinda mlipuko hu una pili aina za sera za kiuchumi na kijamii tutakazoziweka kuhakikisha uchumi unafufuka na kuendelea kuchipuka tena haraka baada ya mlipuko kuisha kwa sababu mambo yanabadilika haraka sana. Tutachapisha ripoti nyingine baada kama ya wiki mbili hivi, na nadhani ni lazima tuwe na uhakika kwamba tunaongeza kasi ya kudhibiti hali hii inayobadilika haraka.”